EU yataka kukomeshwa wimbi jipya la mapigano nchini Sudan
(last modified Mon, 28 Oct 2024 06:47:12 GMT )
Oct 28, 2024 06:47 UTC
  • EU yataka kukomeshwa wimbi jipya la mapigano nchini Sudan

Josep Borrell, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, ameelezea wasiwasi wake kuhusu ripoti za mauaji ya watu wengi na ubakaji katika jimbo la Al-Gezira nchini Sudan.

Katika taarifa yake ya jana kwenye mtandao wa kijamii wa X, Borrel amesema: "Mauaji dhidi ya raia lazima yakomeshwe na wahusika lazima wawajibishwe. EU itaendelea kuchukua hatua ili haki ipatikane."

Sambamba na hilo, Clementine Nkweta-Salami, mratibu mkazi wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya kibinadamu nchini Sudan naye ameelezea wasiwasi wake juu ya kuongezeka mapigano katika eneo hilo.

Amesema: "Nimeshtushwa na kushangazwa sana kwa kuona ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu uliotokea huko Darfur mwaka jana kama vile ubakaji, mashambulizi ya makusudi na mauaji ya watu wengi unarudiwa tena hivi sasa."

Aidha amesisitiza kuwa, mashambulizi dhidi ya raia na miundombinu yanakiuka sheria za kimataifa za kibinadamu na kuongeza kuwa, kulindwa usalama wa raia ni jambo la dharura.

Vita vya uchu wa madaraka baina ya majenerali wa kijeshi wanaoongoza makundi mawili ya SAF na RSF vinaendelea kuinakamisha Sudan kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa. Maelfu ya watu wameshapoteza maisha, mamilioni wamekuwa wakimbizi, kazi zote za maendeleo zimekwama na sehemu kubwa ya miundombinu imeharibiwa huko Sudan.