Mgonjwa 'wa mwisho' wa Marburg Rwanda aruhusiwa kuondoka hospitalini
Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema zaidi ya mwezi mmoja baada ya Rwanda kutangaza mripuko wa ugonjwa wa virusi vya Marburg, hatimaye mamlaka ya afya katika nchi hiyo ya Kiafrika imemruhusu mgonjwa wa mwisho kuondoka hospitalini.
WHO imesema katika taarifa kuwa, mgonjwa wa mwisho aliruhusiwa kuondoka hospitalini siku ya Ijumaa lakini mawasiliano yake, pamoja na yale ya wagonjwa walioruhusiwa hapo awali, yataendelea kufuatiliwa hadi mwisho wa muda wao wa uchunguzi wa siku 21.
Iwapo hakuna maambukizo mapya yanayotokea siku 42 baada ya kesi ya mwisho iliyothibitishwa ya maambukizi, mlipuko huo utatangazwa kuwa umeisha nchini humo.
Jumla ya kesi 66 na vifo 15 vimerekodiwa wakati wa mripuko huo, ambao ulitangazwa mnamo Septemba 27. Waziri wa Afya wa Rwanda, Sabin Nsanzimana amesema mripuko huo umedhibitiwa na ingawa hakuna kesi mpya zinazoripotiwa kwa zaidi ya wiki moja, hatua za ufuatiliaji zinaendelea.
Mapema mwezi uliopita wa Oktoba, Rwanda ilianza kutoa dozi za chanjo ya virusi vya Marburg ili kujaribu kudhibiti mripuko wa ugonjwa huo unaofanana na Ebola katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Brian Chirombo, mwakilishi wa WHO katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki, amesemaa kudhibiti mripuko huo kunatokana na juhudi za pamoja zilizohusisha kupelekwa kwa haraka kwa timu za kukabiliana na ugonjwa huo, ufuatiliaji wa karibu wa mawasiliano, na utekelezaji wa hatua za kuzuia na kudhibiti maambukizi.