Uchaguzi mkuu kufanyika Namibia Jumatano, uwezekano wa rais mwanamke
(last modified Tue, 26 Nov 2024 13:21:52 GMT )
Nov 26, 2024 13:21 UTC
  • Uchaguzi mkuu kufanyika Namibia Jumatano, uwezekano wa rais mwanamke

Raia wa Namibia watapiga kura siku ya Jumatano kumchagua rais mpya na wabunge wa Bunge la Kitaifa katika kinyang'anyiro ambacho wataalamu wanaamini kuwa kinaweza kuwa na ushindani mkubwa zaidi tangu uhuru wa nchi hiyo mwaka 1990.

Netumbo Nandi-Ndaitwah, 72, makamu wa rais wa sasa, anagombea kama mgombea urais wa chama tawala cha SWAPO, ambacho kimekuwa madarakani kwa miaka 34.

Kuna wapiga kura milioni 1.4 waliojiandikisha katika nchi hiyo yenye watu milioni 3.

Vyama 15 vya kisiasa vinachuana kuwania nafasi ya rais na vile vile viti katika Bunge la Kitaifa.

Iwapo Nandi-Ndaitwah atashinda uchaguzi wa Jumatano, ataweka historia kwa kuwa rais wa kwanza mwanamke nchini humo.

Wapinzani wakuu wa Nandi-Ndaitwah ni pamoja na Panduleni Itula wa chama cha IPC, ambaye alifanikiwa kupata asilimia 29.4 ya kura katika uchaguzi wa 2019, ambapo alishindana na hayati Rais Hage Geingob, ambaye alipata asilimia 56.3 ya kura, na kushuka kutoka asilimia 87 ambayo alishinda wakati wa muhula wake wa kwanza mnamo 2014.

Geingob, 82, alifariki mwezi Februari, wiki kadhaa baada ya kutangazwa kuwa anapokea matibabu ya saratani.

Wagombea wengine ni pamoja na McHenry Venaani, kiongozi wa PDM, chama kikuu cha upinzani bungeni, Bernadus Swartbooi wa chama cha LPM, na Job Amupanda.

Kama ilivyo kwa nchi nyingine za Afrika, masuala mengi yanatarajiwa kuathiri uchaguzi wa wapigakura mnamo Novemba 27, ikiwa ni pamoja na ukosefu wa ajira, umaskini, ukuaji duni wa uchumi na ukosefu wa usawa.