Kenya yathibitisha wagonjwa wengine 2 wa Mpox
(last modified Fri, 17 Jan 2025 14:07:05 GMT )
Jan 17, 2025 14:07 UTC
  • Kenya yathibitisha wagonjwa wengine 2 wa Mpox

Kenya leo imethibitisha kuwepo wagonjwa wengine 2 wenye maambukizi ya Mpox na hivyo kufanya jumla ya kesi za ugonjwa huo zilizothibitishwa hadi sasa nchini humo kufikia 33.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya ya Kenya, Mary Muriuki amewaambia waandishi wa habari kuwa wagonjwa hao wawili wamethibitika katika kaunti za Kericho na Taita Taveta na kwamba ugonjwa wa Mpox tayari umeemea katika kaunti 12 za Kenya.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya ya Kenya amesema kuwa Serikali imeimarisha zoezi la kuwafuatilia watu wenye maambukizi kupitia ukaguzi, uchunguzi na kuthibitisha dalili za ugonjwa huo.

Serikali ya Kenya aidha imeanzisha jitihada shirikishi kwa shabaha ya kutoa elimu kwa umma kuhusu hatua za kuzuia na kudhibiti ugonjwa wa Mpox. 

Ugonjwa wa Mpox unaosababishwa na virusi vya familia moja na vile vinavyosababisha ugonja wa ndui (Small Pox), humsababishia mtu homa kali na vidonda juu ya ngozi, kitaalamu kama (vesicles).

Mgonjwa wa Mpox 

Mwaka 2022 milipuko ya Mpox ilizikumba nchi zaidi ya 70. Mwezi Agosti mwaka jana Shirika la Afya Duniani lilitangaza ugonjwa huo kuwa dharuraya afya ya umma. 

Barani Afrika, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inasalia kuwa nchi iliyoathiriwa zaidi, na hadi sasa inaongoza kwa idadi kubwa ya maambukizi yaani watu 49,000. 

Ugonjwa huo wa Mpox umeuwa watu 1,100 katika bara la Afrika tangu Januari mwaka jana.