Niger, Mali na Burkina Faso zajiondoa rasmi ECOWAS
Serikali za kijeshi za Niger, Mali na Burkina Faso zimejiondoa rasmi kwenye Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS).
Kuondoka huko rasmi kumetangazwa na jumuiya hiyo ya kikanda yenye makao yake makuu nchini Nigeria katika taarifa iliyotolewa jana Jumatano.
Katika taarifa hiyo, jumuiya hiyo imesema ilijaribu kuzuia mgawanyiko huo ambao haujawahi kushuhudiwa bila mafanikio, na kusisitiza kwamba "itaacha milango ya ECOWAS wazi" kwa moyo wa "mshikamano wa kikanda".
Nchi wanachama zilizosalia zimetakiwa kuendelea kuwapa raia kutoka nchi hizo tatu fursa na hadhi ya uanachama, ikiwa ni pamoja na usafirishaji huru wa watu na bidhaa.
Julai mwaka jana, nchi tatu hizo za Sahel zilisaini mkataba ulioidhinisha shirikisho zilizounda kati yao, na kujitoa katika jumuiya ya ECOWAS.

Wakuu wa nchi hizo tatu walioingia madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi wamechukua hatua ya kuasisi Muungano wa Sahel (AES) ambao unakusanya watu wasiopungua milioni 72.
Niger, Mali na Burkina Faso zilisema mwezi Januari mwaka huu kwamba zinajitoa katika Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (ECOWAS); jumuiya ambayo wanaituhumu kuwa inahadaiwa na Ufaransa, nchi ya kikoloni.
Nchi zote tatu hizo zimekata uhusiano wao wa kijeshi na kiulinzi na Ufaransa huku zikijikita katika kuanzisha uhusiano mkubwa na Russia.