Kwa nini Afrika Kusini inataka Marekani iwekewe vikwazo
Waziri wa Madini na Rasilimali za Petroli wa Afrika Kusini, Gwede Mantashe ametoa wito kwa nchi za Afrika kusimamisha mauzo ya madini kwenda Marekani.
Mwito huo umetolewa baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kutangaza mipango ya kuikatia misaada Afrika Kusini kutokana na eti sera zake za unyakuzi wa ardhi. Jumapili iliyopita, Trump alidai bila kutoa ushahidi wowote kwamba "matabaka fulani ya watu" nchini Afrika Kusini yanabaguliwa na kunyanyaswa.
Akizungumza katika Kongamano la Uwekezaji wa Madini ya Afrika la Indaba mjini Cape Town, Mantashe amesema kuwa, mataifa ya Afrika hayapaswi kuogopa vitisho vya Marekani. "Tuzuie madini kwenda Marekani," alisema waziri huyo.
Aidha alieleza bayana kuwa, "Kama hawatupi pesa, tusiwape madini ... sisi sio ombaomba, tuitumie jaala hiyo (madini) kwa manufaa yetu. Kama bara iwapo tutadumaa kwa hofu, tutaanguka, lakini na madini mlangoni kwetu.”
Afrika ina takriban 30% ya madini yote duniani. Baadhi ya madini hayo ni kama vile almasi na dhahabu ambayo ni vyanzo vya asili vya utajiri, na vingine hutumiwa katika bidhaa mbalimbali za viwandani kama vile betri na vyombo vya usafiri vya umeme.
Kwa hiyo, utajiri wa Afrika pamoja na nafasi ya kistratijia ya nchi nyingi za bara hilo daima umezifanya nchi za magharibi kuwa na uchu na kwa kutekeleza sera mbalimbali dhidi ya nchi hizo, mbali na kuzikoloni zinufaike na utajiri wa bara hilo.
Hii ni katika hali ambayo, katika miongo ya hivi karibuni nchi nyingi za bara hilo zimeboresha nafasi yao ya kisiasa na kiuchumi katika eneo na katika uga wa kimataifa na zimekuwa na nafasi muhimu na athirifu kimataifa.

Afrika Kusini ni moja ya nchi muhimu za bara la Afrika ambazo zina historia ya mapambano dhidi ya ukoloni na sera ya ukombozi kwa miongo kadhaa, sera ambayo ni shubiri kwa nchi za kikoloni ambazo katu haziko tayari kuistahamili.
Kuhusiana na hilo, mvutano kati ya Marekani na Afrika Kusini umeongezeka katika siku chache zilizopita. Donald Trump ameishutumu Afrika Kusini kwa kukiuka haki za binadamu katika sera ya kuingilia mambo ya ndani ya nchi zingine na ametangaza kuwa atakata misaada yote ya Washington kwa nchi hiyo.
Rais wa Marekani, ambaye ameyapa kipaumbele mashinikizo ya kibabe katika sera zake za kigeni katika muhula wake mpya wa uongozi, wiki iliyopita, katika maamuzi tofauti, alitangaza kutoza ushuru wa 25% kwa bidhaa za Canada na Mexico, na pia kuweka ushuru mpya kwa Uchina. Trump pia ameitishia Ulaya kwamba ataiongozea ushuru wa kibiashara.
Kadhalika Rais wa Marekani amepasisha sera ya vitisho na vikwazo dhidi ya nchi za Afrika, huku akitangaza kusitisha misaada ya kifedha kwa Pretoria kutokana na kile alichokiita ukiukaji wa haki za binadamu.
Hii ni katika hali ambayo, Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini Jumatatu iliyopita alipinga bwabwaja za Trump na kusema kuwa, Pretoria haijawahi kunyakua ardhi yoyote ile. Ramaphosa alisema, kampeni inayofanyika Afrika Kusini ni mchakato wa kisheria ulioidhinishwa kikatiba ambao unataka kuhakikisha kwamba raia wote wanapata ardhi kwa njia sahihi, kiuadilifu na kwa haki kama inavyoelekezwa na katiba.
Pia alifichua kuwa: "Hakuna ufadhili mwingine zaidi ya wa VVU unaopokelewa na Afrika Kusini kutoka Marekani," ikiwa ni kuashiria kwamba amemtaka Trump asiidangaye dunia kwamba Marekani inatoa msaada mkubwa kwa Afrika Kusini na hivyo ina haki ya kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo.

Madai ya Trump yamekuja baada ya Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini kutia saini mwezi uliopita marekebisho ya ardhi kuchukua nafasi ya sheria ya zamani ya kikoloni ya kabla ya mwaka 1975.
Sheria mpya ya ardhi ya Afrika Kusini inaelezea kuwa, mashirika ya serikali yanaweza kunyakua ardhi kwa maslahi ya umma kwa madhumuni mbalimbali.
Ikulu ya Afrika Kusini imesema kuwa mchakato wa sheria hiyo umefanyika kidemokrasia na kikatiba. Demokrasia imekita mizizi Afrika Kusini na utawala wa sheria unaheshimiwa, haki na usawa pia unachungwa nchini humo.
Rais wa Marekani ambaye hivi karibuni alikutana na Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, anajaribu kuchukua hatua za kuilinda Israel na kuzilazimisha nchi zingine zifuate sera za Washington na hivyo kuwa pamoja na Israel.
Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana ametumia sera za Afrika Kusini kama kisingizio cha kuweka mashinikizo kwa nchi hiyo na kuitishia nchi hiyo kuikatia misaada ili iachane na siasa zilizo dhidi ya Israel.
Ukweli wa mambo ni kuwa, Trump anajaribu kuilazimisha Afrika Kusini, ambayo ni miongoni mwa wanachama muhimu wa kundi la BRICS na mwenyekiti wa zamu wa kundi la 20, kutii sera zake inazotaka katika uga wa kisiasa, hususan kukomesha uadui dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.
Lakini msimamo thabiti wa viongozi wa Afrika Kusini kuhusu hatua ya uhasama ya Trump ya kukata misaada ya kifedha ya kupambana na UKIMWI, ambayo si ya kibinadamu unaonyesha kwamba, Pretoria imeazimia kwa moyo imara kupinga ubabe na sera za kibeberu za Washington.