Kutimuliwa wanajeshi wa Ufaransa katika nchi ya sita ya Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i123096-kutimuliwa_wanajeshi_wa_ufaransa_katika_nchi_ya_sita_ya_afrika
Siku ya Alkhamisi, Februari 20, 2025, wanajeshi wa mkoloni kizee wa Ulaya yaani Ufaransa walitimuliwa katika kambi yao pekee ya kijeshi nchini Ivory Coast.
(last modified 2025-02-23T07:34:19+00:00 )
Feb 23, 2025 07:34 UTC
  • Kutimuliwa wanajeshi wa Ufaransa katika nchi ya sita ya Afrika

Siku ya Alkhamisi, Februari 20, 2025, wanajeshi wa mkoloni kizee wa Ulaya yaani Ufaransa walitimuliwa katika kambi yao pekee ya kijeshi nchini Ivory Coast.

Takriban wanajeshi elfu moja wa Ufaransa walikuweko katika kambi iitwayo "Port Bouet" chini ya kivuli cha kukabiliana na ugaidi na kupambana na magenge yenye itikadi kali. Mwezi Disemba 2024, Rais Alassane Ouattara wa Ivory Coast alitangaza kuwatimua wanajeshi wa Ufaransa nchini mwake. Hatua hiyo imechukuliwa kama sehemu ya kuendeleza wimbi la kufukuzwa wanajeshi wa Ufaransa barani Afrika na kupunguza uwepo wa kijeshi wa Paris barani humo.

Ivory Coast ni nchi ya sita barani Afrika iliyotekeleza kivitendo ahadi yake ya kuwatimua wanajeshi wa Ufaransa. Ufaransa kwa sasa ina wanajeshi wake katika nchi mbili tu za Afrika ambazo ni Djibouti;  wanajeshi 1,500; na Gabon wanajeshi 350 wa Ufaransa.

Wanajeshi wa Ufaransa walipotimuliwa nchini Chad

 

Baada ya kumalizika ukoloni na baada ya nchi za Afrika kupata uhuru katika miaka ya 1960, Ufaransa ilishadidisha kuwepo kijeshi katika nchi nyingi za Afrika. Lengo kuu la wakoloni wa Ufaransa lilikuwa ni kuhakikisha kila serikali inayoingia madarakani kwenye nchi hizo za Afrika inakuwa ni kibaraka wa Paris anayelinda maslahi ya mkoloni huyo wa Ulaya barani Afrika. Ni kwa sababu hiyo ndio maana Ufaransa ilikuwa ikishiriki kwenye ya mapinduzi ya mfululizo katika makoloni yake ya zamani. Mkoloni huyo kizee wa Ulaya alichochea mizozo ya kikabila na kisiasa barani Afrika ili nchi hizo za Afrika zisiwe na serikali imara na daima ziwe tegemezi kwa Ufaransa.

Katika kipindi cha miongo sita iliyopita, kumetokea mapinduzi 30 barani Afrika ambapo Ufaransa imekuwa mpangaji mkuu au mfadhili wa mapinduzi hayo. Lengo hasa la kuwepo wanajeshi wa Ufaransa katika nchi kadhaa za Afrika ni kudumisha ushawishi wa kisiasa, kiuchumi na kiusalama wa dola hilo la kikoloni. Lakini hivi sasa hali duniani imebalika. Afrika kama mabara mengine, nayo inaathiriwa na maendeleo ya teknolojia na ushindani wa kimataifa. Hivyo ukoloni mamboleo umepitwa na wakati. Nchi za Kiafrika haziko tayari tena kukubali kutawaliwa na Ufaransa kiuchumi na kisiasa. Waafrika wameelewa kwamba wana nafasi nzuri ya kuanzisha uhusiano wa kuheshimiana na wenye uwiano na madola ya kikanda na kimataifa bila ya kuihitajia kivyovyote vile Ufaransa. Nchi za Afrika zimeelewa pia kwamba, kuendelea na uhusiano na Ufaransa kama ulivyokuwa, ni kwa madhara ya nchi hizo katika kila upande. Bila ya shaka ni kwa sababu hiyo ndio maana nchi za Afrika zinazojiamini, zimeamua kuwatimua wanajeshi wa Ufaransa na kutafuta washirika wapya watakaowawezesha kulinda maslahi ya mataifa yao. Baadhi ya nchi hizo za Afrika zimekwenda mbali zaidi na kuwatimua pia mabalozi wa Ufaransa. Hili kabla ya jambo lolote ni uthibitisho kwamba, enzi ya ushawishi wa kikoloni wa Ufaransa katika makoloni yake ya zamani barani Afrika zimekwisha. 

Afrika imeingia katika zama mpya. Nchi nyingi za Afrika zimeamua kustawisha uchumi wao na kujiletea maendeleo kupitia kuvutia uwekezaji kutoka nchi mbalimbali bila ya kuomba idhini kutoka kwa mkoloni Mfaransa. China na Russia zimewekeza mabilioni ya dola barani Afrika bila ya masharti yoyote; tofauti na unyonyaji wa madola ya Magharibi. Sasa nchi za Afrika hazilazimishwi tena kukabidhi madini yao kwa makampuni ya Ufaransa. Mtazamo kwamba Afrika ni  bara maskini na lenye njaa umebadilika. Afrika sasa ina nafasi muhimu kimataifa. Kupungua ushawishi wa kikoloni wa Ufaransa barani Afrika kuna maana pia ya kupungua nguvu ya Umoja wa Ulaya.