Joto kali lasababisha vifo vya zaidi ya watu 212 barani Ulaya
https://parstoday.ir/sw/news/world-i139430-joto_kali_lasababisha_vifo_vya_zaidi_ya_watu_212_barani_ulaya
Nchi kadhaa za Ulaya zimerekodi vifo vya makumi ya watu kutokana na wimbi kubwa la joto, huku kwa uchache watu 212 wakifariki dunia nchini Uhispania, na wengine kadhaa, wakiwemo watoto 3, wakiaga dunia nchini Ufaransa wiki hii.
(last modified 2026-06-26T04:20:46+00:00 )
Jun 26, 2026 04:08 UTC
  • Joto kali lasababisha vifo vya zaidi ya watu 212 barani Ulaya
    Joto kali lasababisha vifo vya zaidi ya watu 212 barani Ulaya

Nchi kadhaa za Ulaya zimerekodi vifo vya makumi ya watu kutokana na wimbi kubwa la joto, huku kwa uchache watu 212 wakifariki dunia nchini Uhispania, na wengine kadhaa, wakiwemo watoto 3, wakiaga dunia nchini Ufaransa wiki hii.

Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, watu wasiopungua milioni 101 barani Ulaya, wakiwemo zaidi ya milioni 50 nchini Ufaransa na milioni 18 nchini Ujerumani, walitarajiwa kupata halijoto inayozidi nyuzi joto 35 jana Alhamisi.

Takwimu zinaonyesha vifo vya zaidi ya watu 212 vilivyorekodiwa kati ya Jumapili iliyopita na Jumatano wiki hii ambavyo vinaweza kuhusishwa na wimbi la joto lililoikumba Uhispania, kulingana na Taasisi ya Afya ya Carlos III huko Madrid.

Nchini Ufaransa, chanzo cha polisi kiliripoti jana Alhamisi kwamba maiti ya mtoto wa miaka mitatu ilipatikana ndani ya gari katika eneo la Paris, na kumfanya kuwa mtoto wa tatu mwathirika wa wimbi kubwa la joto lililoikumba nchi hiyo wiki hii.

Siku ya Jumatano, Ufaransa ilirekodi siku yake yenye joto kali zaidi tangu vipimo vya halijoto vianze kutumika mwaka wa 1947, ikiwa na wastani wa joto la nyuzi joto 30 Selsiasi.

Mapema jana, Meya wa Paris, Emmanuel Grégoire alitangaza kwamba vifo vinavyosababishwa na joto kali katika mji mkuu vinaongezeka, bila kuweka wazi takwimu maalumu.

Katika mji mkuu, Paris, halijoto ilizidi nyuzi joto 40.3 Selsiasi Jumatano, hii ikiwa ni mara ya nne kuzidi nyuzi joto 40 katika miaka 150.

Nchini Italia, Wizara ya Afya imeweka miji 16 - ikiwa ni pamoja na Florence, Milan, Roma, Turin na Verona - chini ya tahadhari ya juu zaidi ya joto, ikionya kwamba wimbi la joto linaweza kuongezeka zaidi, na kufikia kilele chake Jumapili na Jumatatu.

Halijoto pia inatarajiwa kuzidi nyuzi joto 30 katika maeneo yenye wakazi zaidi ya milioni 70 nchini Ujerumani, milioni 48 nchini Italia, na milioni 38 nchini Uingereza.

Taasisi ya Uchunguzi wa Hali ya Hewa ya Reuters inasema, wimbi kubwa la joto linaloshuhudiwa sasa barani Ulaya linatokana na tukio la hali ya hewa linalojulikana kama Omega Block ambalo limesukuma halijoto hadi nyuzi joto 18 juu ya hali ya kawaida.