Uwezekano wa kutokea vita katika eneo la Maziwa Makuu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i123200-uwezekano_wa_kutokea_vita_katika_eneo_la_maziwa_makuu
Huku vikosi vya waasi wa M23 vikiendelea kusonga mbele katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kumeongeza hatari ya kutokea vita vya pande zote katika eneo la Maziwa Makuu Afrika.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Feb 25, 2025 10:21 UTC
  • Uwezekano wa kutokea vita katika eneo la Maziwa Makuu

Huku vikosi vya waasi wa M23 vikiendelea kusonga mbele katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kumeongeza hatari ya kutokea vita vya pande zote katika eneo la Maziwa Makuu Afrika.

Kundi la waasi la M23 hivi karibuni waliingia katika mji wa Bukavu mashariki mwa Congo baada ya Goma, na wanataka kuendelea kusonga mbele hadi Kinshasa, mji mkuu wa nchi hiyo.

Tangu mwanzoni mwa Januari 2025, waasi wa M23 wamechukua udhibiti wa maeneo kadhaa ya mashariki mwa Kongo, ikiwa ni pamoja na miji ya Goma na Bukavu, na wanaendelea kusonga mbele.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amesema kuwa watu zaidi ya 7,000 wameuawa mwaka huu wakati waasi wa kundi la M23 wanaoungwa mkono na Rwanda wakiteka miji kadhaa katika eneo lenye utajiri wa madini mashariki mwa Kongo.

Judith Tuluka Suminwa ameliambia Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kuwa, hali ya usalama na kibinadamu mashariki mwa Kongo imefikia kiwango cha kutisha.

Viongozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wainaishutumu Rwanda kwamba inawaunga mkono waasi hao, lakini serikali ya Rwanda inakanusha tuhuma hizo na kusema kwamba kundi hilo linafanya kazi chini ya himaya ya serikali ya Kinshasa.

Rais wa Rwanda Paul Kagame, akipinga shutuma za kutekwa kwa nchi hiyo na kundi la M23, alitangaza: "Kuna watu wenye silaha jirani na  Rwanda mashariki mwa nchi hiyo ambao wanatishia maisha ya Wanyarwanda. Watu hawa ni wale wale waliofanya mauaji ya halaiki nchini Rwanda na sasa wakiwa na fikra ileile ya mauaji ya kimbari wako mashariki mwa Congo chini ya uungaji mkono wa serikali ya Kinshasa.

Marais Paul Kagame (kulia) wa Rwanda na Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambao nchi zao zimo katika mzozo mkubwa

 

Kwa hakika maneno ya Rais wa Rwanda yanaashiria kundi linaloitwa "Democratic forces for the liberation of Rwanda" ambao wanatoka kabila la "Wahutu" nchini Rwanda na walihusika katika mauaji ya Watutsi takriban milioni moja nchini humo mwaka 1994.

Licha ya serikali ya Rwanda kukanusha madai ya kuwaunga mkono waasi wa M23 lakini ripoti mbalimbali zikiwemo za Umoja wa Mataifa zinasisitiza uungaji mkono wa Kigali kwa waasi hao.

Filihali hali imezidi kuwa mbaya na maandalizi ya kisiasa na kijeshi kati ya nchi za eneo hilo yameongeza uwezekano wa kutokea vita katika eneo la Maziwa Makuu ya Afrika.

Ukanda huo umekuwa mojawapo ya maeneo yenye mvutano katika bara la Afrika, eneo ambalo linaundwa na nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Rwanda, Burundi, Kenya, Uganda na Tanzania, na kati ya nchi hizi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kwa sababu ya eneo lake la kijiografia na maliasili nyingi, inachukua jukumu kuu katika mvutano wa eneo hilo.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inachukuliwa kuwa moja ya wazalishaji wakubwa wa kobalti, shaba, almasi, dhahabu, mafuta na mbao ulimwenguni. Uwepo wa rasilimali hizi ni moja ya sababu kuu za vita katika eneo hili, kwa sababu vikundi vyenye silaha na serikali tofauti zimekuwa zikishindana na kushiriki katika upatikanaji na udhibiti wa rasilimali hizi. Vikundi tofauti vilivyo na silaha pia hutumia utajiri huu kupata vipato vyao vya kifedha.

Waasi wa M23

 

Kwa upande mwingine, kuna tofauti kubwa za kikabila kati ya nchi mbili za Rwanda na DRC. Mzozo muhimu zaidi wa kikabila na kisiasa katika eneo hilo ni mzozo kati ya makabila ya "Watutsi" na "Wahutu", ambao uliishia kwenye mauaji ya kimbari ya Rwanda mnamo 1994. Wakati huo, maelfu ya Wahutu wa Rwanda walikimbilia Kongo baada ya mauaji ya halaiki dhidi ya Watutsi nchini Rwanda, na jambo hili linaendelea kuchochea vita vikali mashariki mwa Congo.

Majimui ya mazingira  na sababu hizi na uingiliaji ulio nyuma ya pazia wa nchi za Magharibi wa kutaka hisa ya utajiri wa nchi hiyo, hivi sasa umeisukuma hali ya eneo hilo kuelekea kwenye vita kamili, na nchi nyingine za eneo pia zimeingia. Weledi wa mambo wanasema kuwa, endapo hakutachukuliwa hatua za haraka kuupatia ufumbuzi mgogoro huo, kuna uwezekano wa kuibuka vita vya kikanda katika eneo hilo. Ni kwa muktadha huo ndio maana kunatolewa indhari na maonyo mbalimbali na pande tofauti kieneo na kimataifa.

Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye ameonya kuwa mzozo unaoongezeka mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo unaweza kuzusha vita vikubwa zaidi vya kikanda katika eneo la Maziwa Makuu.

Ndayishimiye alisema: "Ikiwa Mashariki mwa Kongo haitokuwa na amani, eneo hilo haliwezi kuwa na amani. Ikiwa itaendelea hivi, kuna hatari ya vita kuenea katika ukanda mzima." na kuongeza kuwa: "Kama Rwanda itaendelea kutaka kuchukua maeneo zaidi na najua vita vitafika hadi Burundi, hatutokubali na vita vitaenea kote na mjiandae kwa matokeo yake."

Burundi iliwatuma wanajeshi wake mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kama sehemu ya kikosi cha Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kuliunga mkono jeshi la Kongo.

Uganda, jirani mwingine wa Kongo, pia ana msimamo wenye utata. Kwa upande mmoja, wanajeshi wa nchi hiyo wapo nchini Kongo na wanapigana na waasi pamoja na jeshi la Kongo. Kwa upande mwingine, kulingana na Umoja wa Mataifa, nchi hii inaunga mkono waasi wa M23.

Maelfu ya watu wameyakimbia makazi yao tangu kuanza mwaka huu (2025) kufuatia kusonga mbele waasi wa M23 katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo

 

Wakati huo huo, mamilioni ya watu wasio na ulinzi mashariki mwa Kongo wanakabiliwa na ghasia mbaya, kuhama makazi na ukosefu wa mahitaji ya kimsingi ya maisha na hivyo kuibua wasiwasi wa kutokea janga la kibinadamu.

Hivi karibuni Umoja wa Afrika ulitahadharisha kuhusu kuchukua wigo mpana vita vya mashariki mwa DRC na kuenea katika eneo lote la Maziwa Makuu na kutangaza kwamba, kuzuka kwa vita katika eneo hilo kunaweza kusababisha kuenea kwa migogoro ya kibinadamu na kiuchumi na hata kufikia viwango vya kimataifa.

Ala kulli haal, inaonekana kuwa ili kuzuia kuenea kwa mgogoro huo na kuepusha kutokea vita katika eneo la Maziwa Makuu barani Afrika, kuna haja ya kuchukuliwa hatua za dharura na madhubuti kutoka kwa jamii ya kimataifa kwa ushirikiano na serikali za eneo hilo.