Mali na Russia zajadili kuimarisha ushirikiano wa kiulinzi
Ujumbe wa ngazi ya juu wa Russia ukiongozwa na Naibu Waziri wa Ulinzi, Yunus-Bek Yevkurov umeitembelea Mali na kufanya mazungumzo na maafisa wa taifa hilo la Afrika Magharibi, kuhusu kuimarisha ushirikiano wa usalama na ulinzi wa pande mbili.
Safari ya Yevkurov nchini Mali inakuja baada ya kutia saini makubaliano ya ushirikiano wa kijeshi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati wakati wa ziara yake mwishoni mwa Februari. Rais wa mpito wa Mali, Jenerali Assimi Goita, aliupokea ujumbe huo wa Russia na kufanya mazungumzo kuhusu uhusiano wa pande mbili, ofisi yake ilitangaza katika taarifa fupi siku ya Jumatano.
Shirika la habari la Russia la 'African Initiative' limeripoti kuwa mazungumzo kati ya Yevkurov na Waziri wa Ulinzi wa Mali, Sadio Camara yalijikita juu ya hali ya usalama katika eneo la Sahel barani Afrika
Kwa mujibu wa African Initiative, pande hizo pia zimejadili utekelezaji wa makubaliano ya pande mbili yaliyotiwa saini hapo awali juu ya ushirikiano wa kijeshi na kiufundi.
Eneo la Kaskazini mwa Mali kimekuwa kitovu cha uasi mbaya wa wanamgambo katika eneo la Sahel, ambao ulizuka mwaka 2012 na umeenea hadi nchi jirani za Niger na Burkina Faso.
Vifo vilivyoripotiwa katika nchi tatu hizo za Afrika Magharibi vilifikia kiwango cha juu cha 7,620 katika nusu ya kwanza ya 2024 pekee, kwa mujibu wa shirika la Armed Conflict Location and Event Data.