Sudan yaishukuru UNSC kwa kupinga kuundwa serikali nyingine nchini humo
Serikali ya Jenerali Abdul Fattal al Burhan wa Sudan imetangaza kufurahishwa na taarifa ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) ya kupinga juhudi za kuundwa serikali nyingine sambamba na ile inayotawala hivi sasa nchini Sudan.
Hayo yamo kwenye taarifa ya Khalid Ali Aleisir, Waziri wa Habari wa Sudan ambaye pia ni msemaji wa Serikali. Amesema: "Serikali ya Sudan inakaribisha taarifa ya UNSC ya kupinga kutiwa saini mkataba unaolenga kuunda serikali nyingine sambamba na iliyopo hivi sasa humu nchini."
Waziri wa Habari wa Sudan amekariri kujitolea serikali ya nchi hiyo katika kupigania amani na kuhakikisha mgogoro wa vita wa nchi hiyo unamalizwa, umoja na uadilifu unalindwa katika kila shibri ya ardhi ya Sudan na matarajio ya wananchi yanatimizwa hasa yanayohusiana na usalama, demokrasia na maendeleo.
Aidha amesisitizia umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika kusaidia walioathirika na vita hivyo akitilia mkazo dhamira ya serikali ya nchi yake ya kuwezesha juhudi za usambazaji wa misaada ya kibinadamu.
Pia amepinga vikali Sudan kuingiliwa na mataifa ya kigeni ambayo yanaweza kuyumbisha usalama wa nchi na eneo hilo zima. Tayari serikali ya Sudan imefungua kesi dhidi ya Umoja wa Falme za Kiarabu katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki kwa madai ya kuingilia masuala ya ndani ya Sudan, kushiriki katika mauaji ya kimbari na kuvipa silaha Vikosi vya Msaada wa Haraka RSF.
Siku ya Jumatano, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilitoa taarifa iliyoonesha "wasiwasi mkubwa" wa baraza hilo kuhusu suala la kutiwa saini mkataba wa kuanzisha serikali nyingine nchini Sudan sambamba na iliyopo hivi sasa.