Mkuu wa Jeshi: Iran haitachoka kuwafuatilia waliomuua Kiongozi wetu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i139676-mkuu_wa_jeshi_iran_haitachoka_kuwafuatilia_waliomuua_kiongozi_wetu
Iran haitawahi kuacha azma yake ya kutafuta haki na kulipiza kisasi dhidi ya wauaji wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Shahidi Ayatullah Ali Khamenei (Mwenyezi Mungu amrehemu), zaidi ya miezi minne tangu alipouawa shahidi katika mashambulizi ya kigaidi ya Marekani na Israel.
(last modified 2026-07-06T03:51:04+00:00 )
Jul 06, 2026 03:50 UTC
  •  Mkuu wa Jeshi la Iran, Meja Jenerali Amir Hatami
    Mkuu wa Jeshi la Iran, Meja Jenerali Amir Hatami

Iran haitawahi kuacha azma yake ya kutafuta haki na kulipiza kisasi dhidi ya wauaji wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Shahidi Ayatullah Ali Khamenei (Mwenyezi Mungu amrehemu), zaidi ya miezi minne tangu alipouawa shahidi katika mashambulizi ya kigaidi ya Marekani na Israel.

Kauli hiyo imetolewa Jumapili na Mkuu wa Jeshi la Iran, Meja Jenerali Amir Hatami, katika siku ya pili ya mazishi ya umma ya Ayatullah Khamenei na wanafamilia wake waliouawa shahidi katika hujuma hiyo ya kigaidi.

Jenerali Hatami amesema: “Wale waliofanya uhalifu huu lazima wajue kuwa taifa la Iran, na sisi sote, hatutaacha kamwe jitihada zetu za kutafuta haki. Hatutawaacha wapotee, na huu ni uamuzi thabiti ambao tutaufuata mpaka tutakapopata matokeo yanayostahili."

Ayatullah Khamenei, pamoja na binti yake, mkwe wake, mke wa mwanawe, mjukuu wake, na makamanda kadhaa wa juu wa kijeshi, waliuawa shahidi kidhalimu katika shambulio lililolenga ofisi yake jijini Tehran mnamo Februari 28 sawa na 10 Ramadhani, katika siku ya kwanza ya vita vya siku 40 vya Marekani na Israel dhidi ya Iran.

Ukatili huo ulizua majibu makubwa kutoka kwa Iran, ikiwemo mashambulizi dhidi ya vituo vya kijeshi na rasilimali za Marekani katika eneo, pamoja na mashambulizi ya makombora dhidi ya maeneo yanayokaliwa na Israel.

Hata hivyo, wakuu wa Iran na wananchi wamekuwa wakisisitiza mara kwa mara kuwa nchi hii inafuatilia kulipiza kisasi cha mwisho kwa mauaji ya Ayatullah Khamenei, mwanazuoni mpendwa na kielelezo cha imani kwa Waislamu ulimwenguni kote.

Kiongozi Shahidi alikuwa na umri wa miaka 86 wakati alipouawa shahidi na alikuwa mhimili wa pili muhimu katika historia ya Iran baada ya Mapinduzi, akimfuata mwanzilishi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Khomeini (RA), mnamo mwaka 1989.

Mamilioni ya waumini na wananchi wamekuwa wakijitokeza kwa wingi katika Ukumbi wa Mosalla jijini Tehran ili kuaga mwili wa Ayatullah Khamenei na wanafamilia wake.

Mwili wa Ayatullah Khamenei utapumzishwa katika Haram takatifu la Imam Ridha (AS) mjini Mashhad kaskazini mashariki mwa Iran, mji wake wa kuzaliwa, siku ya Alhamisi, baada ya mchakato wa siku tatu wa misafara ya mazishi kuanzia Tehran, Qom, na nchini Iraq katika miji ya Najaf na Karbala.