Jeshi la Nigeria: Tumeangamiza magaidi 92, tumetia mbaroni 111
Katika taarifa yake ya karibuni zaidi, jeshi la Nigeria limetangaza kuwa, limeangamiza takriban magaidi 92 na kuwatia mbaroni wengine 111 katika operesheni mbalimbali za wanajeshi wa nchi hiyo kwenye kipindi cha wiki moja iliyopita.
Markus Kangye, Msemaji wa Jeshi la Nigeria amesema hayo mbele ya vyombo vya habari huko Abuja, mji mkuu wa Nigeria wakati akitoa taarifa kuhusu hali ya usalama nchini humo na kusema: Operesheni za nchi nzima dhidi ya "wahalifu" zimekuwa na mafanikio makubwa.
Taaarifa hiyo imeongeza kuwa, magaidi 101 wamejisalimisha kwa vikosi vya ulinzi na usalama vya Nigeria wakati wa operesheni hizo.
Amebainisha kuwa, mateka 75 wamekombolewa kutoka mikononi mwa wahalifu katika kipindi cha operesheni hizo, akiongeza kuwa wanajeshi wa Nigeria wamefanikiwa pia kukamata silaha 117 za aina mbalimbali na risasi 2,939.
Akiendelea na taarifa yake, Msemaji wa Jeshi la Nigeria, Markus Kangye amesema kuwa, katika kipindi cha wiki iliyopita, wanajeshi wa nchi hiyo wamewatia mbaroni takriban wezi 18 wa mafuta na kuzuia operesheni nyingi za wizi wa mafuta katika eneo la Delta.
Ameongeza kuwa, takriban lita 452,396 za mafuta ghafi ya wizi, lita 224,175 za mafuta ya magari yaliyosafishwa kinyume cha sheria na lita 1,920 za petroli zimekatwa wakati wa operesheni hizo.