UNHCR: Wakimbizi wasiopungua 63,000 wa DRC wameingia Burundi
Zaidi ya watu 63,000 hadi sasa wameingia Burundi wakikimbia machafuko nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Hayo ni kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) ambalo limesema wengi wao wanaishi katika hali ngumu ndani ya uwanja wa michezo wa Rugombo jimboni Cibitoke huku wakisubiri kuhamishiwa kwenye kambi rasmi za wakimbizi.
Katika uwanja wa michezo wa Rugombo ambao umegeuka makazi ya muda ya wakimbizi ni vigumu kuutambua kama ni uwanja wa michezo kwani umesheheni mahema kila kona.
Wanawake, watoto na wanaume waliokimbia vita DRC wamefika hapo kusaka usalama na kunusuru maisha yao.
UNHCR inasema katika mazingira ya sasa ya ufadhili finyu, Burundi ni moja ya nchi zinazohitaji msaada wa haraka ikiwa ni pamoja na makazi bora kwa wakimbizi, chakula na maji safi, huduma za afya, usafi wa mazingira na ulinzi kwa wanawake na watoto walio hatarini zaidi.
Aline Irakarama, afisa habari msaidizi wa UNHCR Burundi anasema wanajitahidi wawezavyo “UNHCR, kwa kushirikiana na serikali ya Burundi, inaendelea na mchakato wa kusajili wakimbizi wapya, hasa watoto wasio na walezi na waliotenganishwa na familia zao. Lengo ni kuhakikisha wanapata ulinzi na huduma muhimu.
Baada ya usajili, wakimbizi hawa watahifadhiwa katika kambi ya wakimbizi ya Musenyi, iliyopo katika mkoa wa Rutana, mbali na mpaka.
UNHCR imeonya kwamba bila ufadhili wa kutosha, maisha zaidi ya wakimbizi yako hatarini hivyo imeihimiza jamii ya kimataifa kutoa msaada wa haraka ili kuzuia janga kubwa zaidi la kibinadamu.
Kundi la M23 limezidisha udhibiti wa eneo la mashariki mwa DRC tangu Disemba mwaka uliopita, na kutwaa miji ya Goma na Bukavu. Serikali ya DRC inaituhumu Rwanda kuwa inawaunga mkono waasi hao. Rwanda imekanusha tuhuma hizo