IOM: Wahamiaji 563 wamekamatwa katika pwani ya Libya
Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) lilitangaza Jumatatu kwamba wahamiaji 563 wamekamatwa kando ya pwani ya Libya katika kipindi cha wiki moja iliyopita.
Miongoni mwa wahamiaji hao, kulikuwa na wanawake 43 na watoto 12, huku pia mwili wa mtu mmoja aliyefariki ukipatikana.
Kulingana na takwimu za IOM, katika mwaka huu pekee, jumla ya wahamiaji 4,767 wamekamatwa na kurejeshwa Libya, huku 82 wakiripotiwa kufariki na wengine 58 kutoweka katika njia ya Mediterania.
Kutokana na hali ya ukosefu wa usalama na machafuko nchini Libya tangu kutumuliwa madarakani na kuuawa Muammar Gaddafi mwaka 2011, wahamiaji wengi, hasa kutoka Afrika, huchagua kuvuka Bahari ya Mediterania kuelekea Ulaya kupitia Libya.
Wiki iliyopita, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Libya Emad al-Tarabelsi alisisitiza umuhimu wa msaada kutoka Umoja wa Mataifa ili kuharakisha mpango wa kuwarejesha wahamiaji kwa hiari katika nchi zao za asili.
Hata hivyo, al-Tarabelsi ameonya kuwa Libya inaweza "kuwafukuza kwa nguvu wahamiaji haramu" endapo jamii ya kimataifa itashindwa kusaidia mchakato wa kurejesha wahamiaji hao kwa hiari katika mataifa yao.