Tunisia na Misri kwa mara nyingine zapinga kuhamishwa kwa nguvu Wapalestina
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i123774-tunisia_na_misri_kwa_mara_nyingine_zapinga_kuhamishwa_kwa_nguvu_wapalestina
Rais Abdel-Fattah al-Sisi wa Misri na mwenzake wa Tunisia, Kais Saied, wametilia tena mkazo msimamo wa nchi zao wa kupinga kuhamishwa kwa nguvu Wapalestina katika ardhi zao.
(last modified 2025-03-11T07:56:02+00:00 )
Mar 11, 2025 07:56 UTC
  • Tunisia na Misri kwa mara nyingine zapinga kuhamishwa kwa nguvu Wapalestina

Rais Abdel-Fattah al-Sisi wa Misri na mwenzake wa Tunisia, Kais Saied, wametilia tena mkazo msimamo wa nchi zao wa kupinga kuhamishwa kwa nguvu Wapalestina katika ardhi zao.

Viongozi hao wawili wamefanya mazungumzo ya simu na kujadiliana hali ya Ukanda wa Ghaza na kupitia tena mapendekezo ya Misri ya kuhakikisha mapigano yanasimamishwa kikamilifu na misaada ya kibinadamu inafikishwa kwa wananchi wa Ghaza kiukamilifu kama vinavyosema vipengee vya makubaliano ya kusimamisha vita kati ya HAMAS na Israel.

Taarifa hiyo imesema pia kuwa rais wa Tunisia amepongeza mapendekezo ya Misri kuhusu kuijenga upya Ghaza. Mpango huo ulipasishwa kwa kauli moja kwenye mkutano wa dharura wa hivi karibuni wa nchi za Kiarabu. Rais wa Tunisia amesisitiza kuwa, nchi yake inaunga mkono kikamilifu mpango huo kwani lengo la mpango huo ni kuijenga upya Ghaza bila ya kuwafukuza wakaazi wake.

Marais wa Misri na Tunisia wamesisitiza pia kwamba kuanzishwa nchi huru ya Palestina kwenye mipaka ya mwaka 1967, huku Baytul Muqaddas ukiwa mji mkuu wake, bado ndiyo njia pekee ya kuwezesha kupatikana amani ya kudumu katika ukanda huu mzima.

Mazungumzo ya simu baina ya marais wa Misri na Tunisia yamezungumzia pia matukio ya nchi nyingine za Kiarabu hasa Libya na Syria, huku marais wote hao wawili wakisisitiza kuwa, wataendelea kujitolea kupigania utulivu, umoja na mshikamano wa ardhi zote za nchi za eneo hili bila ya ubaguzi na kuhakikisha matatizo yote yanatatuliwa kwa njia ya mazungumzo.