ANC: Afrika Kusini haitakubali Kutishwa na Marekani
Naibu Katibu Mkuu wa kwanza wa chama tawala cha Afrika Kusini, ANC, Nomvula Mokonyane, amekemea wanachama wa chama cha Democratic Alliance (DA) ambao wamekwenda Marekani kujipendekeza kwa rais wan chi hiyo Donald Trump na kutaja hatua hiyo kama dharau kwa uhuru wa nchi hiyo.
Akizungumza pembezoni mwa mkutano wa chama hicho uliofanyika Free State, Mokonyane ameunga mkono kauli ya Rais Cyril Ramaphosa kwamba Afrika Kusini haitakubali kutishwa na Marekani.
Mokonyane alieleza kuwa Afrika Kusini si adui wa Marekani, kama Wamarekani wanavyodai, lakini ilibainisha wazi kuwa hawatakubali vitendo vya ubabe.
Hivi karibuni, wanachama wa chama cha DA walifanya ziara ya kazi ya wiki moja nchini Marekani ili kukutana na utawala wa Trump kwa ajili ya kujadili mahusiano ya kidiplomasia kati ya Afrika Kusini na Marekani.
ANC imetangaza kuunga mkono kikamilifu Rais Ramaphosa na Waziri wa Mahusiano ya Kimataifa Ronald Lamola katika juhudi zao za kusimamia mahusiano yenye mvutano kati ya Marekani na Afrika Kusini.
Mokonyane pia alisifu serikali ya Afrika Kusini kwa jinsi inavyoshughulikia suala hilo, akisema kuwa hatua zilizochukuliwa ni za busara na za kidiplomasia.
Serikali ya Afrika Kusini imeeleza kuwa Donald Trump ana uelewa usio sahihi kuhusu sheria mpya ya ardhi nchini humo. Sheria hii inaruhusu kuchukuliwa ardhi bila fidia katika baadhi ya hali.