UNICEF: Watoto Sudan wanakabiliwa na machungu yasiyoelezeka
Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Catherine Russell, amesema vita vinavyoendelea Sudan ni janga kubwa zaidi la kibinadamu duniani, likiwaacha watoto katika hali mbaya zaidi.
Akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa siku y Alhamisi, Bi. Russell amesema zaidi ya watu milioni 30, nusu yao wakiwa watoto, wanakumbwa na ukatili, njaa, na magonjwa hatari tangu mapigano yaanze Aprili 2023 kati ya jeshi la Sudan (SAF) na waasi wa RSF.
Takriban watu milioni 12 wamekimbia makazi yao, huku miundombinu muhimu, ikiwemo hospitali, ikiharibiwa. UNICEF imeripoti visa vya kutisha vya ukiukwaji wa haki za watoto, ikiwa ni pamoja na mauaji, ukatili wa kingono, na kulazimishwa kujiunga na makundi yenye silaha. Kati ya Juni na Desemba 2024, zaidi ya matukio 900 ya ukiukwaji mkubwa wa haki za watoto yalirekodiwa, asilimia 80 yakiwa mauaji au ulemavu wa kudumu.
Zaidi ya watoto 770,000 wanatarajiwa kuathirika na utapiamlo mkali mwaka huu, huku misaada ya kibinadamu ikikumbwa na vikwazo vya kiutawala na usalama. Bi. Russell ameitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua za haraka kuwalinda watoto, kuruhusu misaada ipatikane bila vikwazo, na kuwawajibisha wanaohusika na ukiukwaji wa haki. UNICEF inahitaji dola bilioni 1 kusaidia watoto milioni 8.7 walioko hatarini Sudan.
Sudan ilitumbukia kwenye mgogoro mbaya baada ya wanamgambo wa RSF kutaka wapate nafasi zaidi serikalini. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, hadi hivi sasa mapigano hayo yameshaua watu 29,683.
Kwa upande wake, Shirika la Kimataifa la Uhamiaji limesema kuwa, mgogoro wa Sudan umewakosesha makazi zaidi ya watu milioni 15 ndani na nje ya nchi hiyo.
Serikali ya Sudan imetangaza RSF kuwa kundi la kigaidi linatolekeleza jinai na mauaji ya kimbari.