Wahamiaji 194 wa Kiafrika wakamatwa nchini Yemen
Vikosi vya usalama vya Yemen jana viliwatia mbaroni wahamiaji 194 kutoka eneo la Pembe ya Afrika waliokuwa wakijaribu kuingia nchini humo kinyume cha sheria kupitia mkoa wa Shabwa wa kusini mashariki mwa nchi hiyo.
Polisi wa eneo hilo wamewatia mbaroni wahamiaji hao walipokaribia fukwe za Yemen wakiwa ndani ya meli katika wilaya ya Radhum ya mkoa wa Shabwa,
Hayo yametangazwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Yemen katika taarifa yake rasmi kwa kwa vyombo vya habari na kuongeza kuwa, miongoni mwa wanaoshikiliwa ni Waethiopia 121 -- wanawake 70, wanaume 46 na watoto watano -- pamoja na Wasomali 73, wengi wao wanaume.
Wizara hiyo imeongeza kwa kusema: Mamlaka za usalama ya Yemen zimefungua kesi za kisheria dhidi ya watu hao kwa kuingia nchini humo kinyume cha sheria.
Njia ya baharini kutoka eneo la Pembe ya Afrika kuelekea Yemeni ni hatari sana. Wahamiaji mara nyingi wanasafiri kwa meli zilizojaa na zisizo na uwezo wa kuhimili mawimbi makubwa ya baharini. Meli hizo ni za kifo kwani zinaendeshwa na wasafirishaji haramu ambao wamejitolea roho zao kwa hatari yoyote ile. Wahamiaji wanaotumia njia hiyo kwa kawaida wanakusudia kufikia nchi za Ghuba ya Uajemi kusaka ajira.
Kwa mujibu wa ripoti za awali za Umoja wa Mataifa, wahamiaji 60,897 wa Kiafrika waliingia Yemen mwaka jana baada ya kufanya safari za hatari za baharini.