Kagame akosoa kimya cha Magharibi kuhusu FDLR; aisuta Ubelgiji
Rais wa Rwanda, Paul Kagame amezikosoa vikali nchi za Magharibi kwa kueneza 'simulizi potofu' kwamba Kigali inawaunga mkono waasi wa M23 huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Akihutubia mkutano wa hadhara katika mji mkuu wa nchi hiyo Kigali, Kagame amesema nchi za Magharibi zinaeneza 'propaganda' kwamba Rwanda inaunga mkono na kufadhili shughuli za M23, huku zikifumbia macho ukweli kwamba Kinashasa inaliunga mkono kundi la waasi wa Kihutu la Democratic Forces for the Liberation of Rwanda (FDLR).
Amesema, "Tumeiambia dunia nzima kuhusu wasiwasi wetu juu ya hawa Intarahamwe na mashambulizi wanayoyafanya dhidi yetu, lakini wanaendelea kupuuza na kusema hao (FDLR) ni wachache."
Kadhalika Kagame ameishutumu Ubelgiji kwa kushinikiza vikwazo vya kimataifa dhidi ya Rwanda kutokana na mzozo wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Amesema mkoloni huyo wa zamani wa nchi hiyo amekuwa na mtindo wa muda mrefu wa kuidogosha Rwanda. “Wanazungumza kuhusu vita vya Kongo, kwanza wanavifanya kuwa ni vita vya Rwanda, halafu wanadai kwamba Rwanda inaviunga mkono,” amesema.

Kagame amedai kuwa Ubelgiji ilimega sehemu kubwa ya ardhi ya Rwanda na kuipa Kongo enzi za ukoloni, ili Rwanda ionekane ndogo kama Ubelgiji.
Kongo na nchi za Magharibi zinaituhumu nchi jirani ya Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23, madai ambayo Kigali imeyakanusha vikali.