Libya yaitaka jamii ya kimataifa kuisaidia mzigo wa wakimbizi
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Libya, Emad al-Tarabelsi, ametoa mwito kwa jamii ya kimataifa ukiwemo pia Umoja wa Ulaya kuisaidia mzigo wa wakimbizi haramu wanatumia ardhi ya Libya kujaribu kuelekea barani Ulaya.
Al-Tarabelsi aliyasema hayo wakati wa mkutano uliofanyika katika mji mkuu wa Libya, Tripoli kati yake na Balozi wa Umoja wa Afrika na yule wa Umoja wa Ulaya nchini Libya, pamoja na wawakilishi wa Ujumbe wa Umoja wa Ulaya. Hayo yamo kwenye taarifa ya pamoja ya Shirika la Kimataifa la Uhamiaji na shirika la kuhudumia wakimbizi la UNHCR.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Libya ameutaka Umoja wa Ulaya na nchi zilizoathiriwa na uhamiaji haramu kutoa usaidizi madhubuti kwa Libya kwa kuimarisha usalama kwenye mipaka yake ya kusini, kutoa vifaa na teknolojia za kisasa za kufuatilia mienendo haramu, kuharakisha kuwarejesha makwao wahamiaji haramu sambamba na kupambana na magendo na biashara haramu ya binadamu.
Waziri huyo amebainisha kuwa, Libya haitabeba mzigo wa uhamiaji haramu peke yake na kamwe haitakuwa eneo la makazi (kwa wahamiaji), akionya kwamba kuendelea kumiminika bila ya kudhibitiwa wahamiaji hao kutazidisha hatari za kiusalama na kijamii, sio tu nchini Libya bali katika eneo hilo lote. Aidha Libya imesisitizia ulazima wa kuanzishwa miradi ya maendeleo katika nchi ambazo ni chanzo kikuu cha wahamiaji haramu.
Wahamiaji wengi hasa kutoka nchi za Afrika za kusini mwa Jangwa la Sahara, wanatumia ardhi ya Libya kuvuka Bahari ya Mediterania kuelekea Ulaya kwa sababu ya ukosefu wa usalama na machafuko nchini humo tangu ulipoangushwa utawala wa Muammar Gaddafi mwaka 2011.