Amiri wa Qatar awakutanisha viongozi wa DRC na Rwanda huku mvutano ukishadidi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i124104-amiri_wa_qatar_awakutanisha_viongozi_wa_drc_na_rwanda_huku_mvutano_ukishadidi
Amiri wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani amewaleta pamoja viongozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Rwanda kwa lengo la kutuliza hali mashariki mwa DRC. 
(last modified 2025-03-19T08:20:14+00:00 )
Mar 19, 2025 08:20 UTC
  • Amiri wa Qatar awakutanisha viongozi wa DRC na Rwanda huku mvutano ukishadidi

Amiri wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani amewaleta pamoja viongozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Rwanda kwa lengo la kutuliza hali mashariki mwa DRC. 

Katika taarifa Jumanne, Ofisi ya Amiri ilisema Sheikh Tamim alikutana na Rais wa DRC Felix Tshisekedi na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame katika Kasri la Lusail mjini Doha.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa: Viongozi wote watatu wamekubaliana juu ya haja ya kuendelea na mazungumzo yaliyoanzishwa Doha ili kuweka misingi imara ya amani ya kudumu kama ilivyotarajiwa katika mchakato wa Luanda/Nairobi." 

Mkutano wa Qatar, ambao haukutrajiwa,  ulifanyika Jumanne,  siku ambayo Angola ilitangaza kufuta mazungumzo ya DRC na waasi wa M23  baada ya wawakilishi wa M23 kujiondoa katika mkutano huo. 

Viongozi hao wawili pia walimshukuru Amiri wa Qatar kwa kuandaa “mkutano wenye matokeo mazuri, ambao umesaidia kujenga imani katika kujitolea kwa pamoja kwa ajili ya mustakabali wa usalama na utulivu” wa DRC na ukanda mzima.

Mazungumzo hayo mjini Doha yameashiria mkutano wa kwanza wa ana kwa ana kati ya marais hao wawili tangu waasi wa M23 walipoanzisha mashambulio mashariki mwa DRC ambapo waliteka miji mikubwa ya Goma na Bukavu. 

DRC inasema zaidi ya watu 7,000 wameuawa katika eneo hilo tangu mwanzo wa mwaka.

Umoja wa Mataifa na DRC kwa muda mrefu zimeishutumu Rwanda kuwa inawaunga mkono waasi wa M23—madai ambayo Kigali imeyakanusha mara kwa mara