Rais wa Somalia anusurika jaribio la mauaji la magaidi wa al-Shabaab
Serikali ya Somalia imetangaza kuwa mlipuko uliofanyika Jumanne mjini Mogadishu ulikuwa jaribio la kumuua rais wa nchi hiyo ambalo limetekelezwa na kundi la kigaidi la al-Shabaab.
Wizara ya Habari ilisema msafara wa Rais Hassan Sheikh Mohamud ulikumbwa na shambulio karibu saa nne na nusu asubuhi katika wilaya ya Xamar-Jajab mjini Mogadishu.
Taarifa hiyo imesema Mohamud alikuwa njiani kuelekea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mogadishu kwa ajili ya kutemeblea wanajeshi walioko mstari wa mbele vitani katika jimbo la Hirshabelle.
Taarifa hiyo imesema: “Shambulio hilo lilizimwa, na Rais alifika salama katika sehemu ya mwisho kama ilivyopangwa.”
Wizara hiyo imeongeza kuwa “kitendo hiki cha woga kilichosababisha vifo na majeruhi ya raia wasio na hatia” ni ushahidi wa kukata tamaa kwa kundi hilo ambalo limeshindwa mara kadhaa mikononi mwa Jeshi la Kitaifa la Somalia."
Vikosi vya usalama vimeanzisha uchunguzi kuhusu shambulio hilo ambalo lilifanyika karibu na eneo lenye ulinzi mkali katika mji mkuu.
Taarifa hiyo pia imebaini kuwa: “Kwa umoja wa watu wetu na msaada wa washirika wetu wa kimataifa, tutaleta amani na utulivu wa kudumu Somalia."
Hussien Sheikh Ali, mshauri wa rais wa masuala ya usalama wa kitaifa, amesema kuwa rais yuko salama na yuko katika miji ya mstari wa mbele wa mapambano dhidi ya magaidi.
Aidha amesema: “Taifa hili haliwezi kutishwa na unafiki na uwongo uliopindukia."
Kundi la kigaidi la al Shabab linalofungamana na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda, al-Shabaab, lilidai kuhusika na shambulio hilo, likisema kuwa liliushambulia msafara wa rais uliokuwa ukielekea uwanja wa ndege.