Rwanda yakaribisha uamuzi wa waasi wa M23 kuondoka katika mji wa Walikale
Viongozi wa Rwanda wamekaribisha hatua ya waasi wa M23 ya kuondoka katika mji wa kistratejia na wenye utajiri wa madini wa Walikale na kukaribisha pia juhudi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo za kusitisha uhasama katika mzozo unaoendelea mashariki mwa nchi hiyo.
Taarifa kutoka ofisi ya Msemaji wa serikali ya Rwanda imeeleza kuwa Rwanda inaunga mkono ubunifu kwa ajili ya kupatikana ufumbuzi wa kudumu wa kisiasa na kiusalama kwa mgogoro wa mashariki mwa Kongo.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa: Rwanda inakaribisha tangazo la waasi wa M23 la kuondoa wapiganaji wake katika mji wa Walikale mashariki mwa Kongo ili kuunga mkono jitihada za kusaka amani zinazoendelea kutekelezwa na pia inakaribisha tangazo la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwamba operesheni zote za mashambulizi za FARDC (vikosi vya serikali) na kundi la Wazalendo (wanamgambo wanaounga mkono serikali) zitasitishwa.
Baada ya waasi wa M23 kutangaza kuondoka katika mji wa kistratejia waliokuwa wameuteka wa Walikale; jeshi la Kongo pia kwa upande wake limesema kuwa limevitaka vikosi vyake vya ulinzi kupunguza kasi ya mashambulizi ili kutoa kipaumbele kwa mazungumzo ya amani na kuendelea mchakato wa mazungumzo ya Luanda na Nairobi.
Waasi wa M23 wameyateka maeneo mengi ya majimbo ya Kivu Kaskazini na Kusini tangu washadidishe hujuma zao dhidi ya maeneo mbalimbali mashariki mwa Kongo mwaka jana.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na baadhi ya nchi zinaituhumu Rwanda kuwa inawaunga mkono waasi wa M23, hata hivyo Kigali, inakanusha madai hayo.