Baraza la Usalama lalaani kushambuliwa walinda amani wa UN nchini CAR
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limelaani shambulizi lililofanywa dhidi ya askari wa kulinda amani wa umoja huo huko Jamhuri ya Afrika ya Kati. Askari mmoja raia wa Kenya ameuawa kwenye shambulio hilo.
Timu ya Umoja wa Mataifa ya Kuleta Utulivu wa pande nyingi huko Jamhuri ya Afrika ya Kati imesema kwamba askari wa kulinda amani wa umoja huo walishambuliwa na kundi lisilojulikana lenye silaha wakati walipokuwa wanafanya doria ya masafa marefu katika kijiji cha Tabane, Mkoa wa Haut-Mbomou.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Baraza la Usalama limetoa salamu za rambirambi rambirambi kwa familia ya askari huyo aliyeuawa pamoja na taifa la Kenya na Umoja wa Mataifa.
Baraza hilo limesisitiza kuwa mashambulizi dhidi ya askari wa kulinda amani huenda yakajumuisha uhalifu wa kivita na kuzitanabahisha pande zote kwamba zina wajibu wa kuchunga vitendo vyao kwani vinafuatiliwa na sheria za kimataifa za kibinadamu.
Kabla ya taarifa hiyo ya Baraza la Usalama, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres naye alikuwa tayari ameshalaani vikali shambulio hilo na kuwataka viongozi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati kufanya juhudi zao zote kuhakikisha wanawasaka na kuwatia mbaroni wahusika wa shambulio hilo ili wafikishwe mahakamani haraka na sheria ifuate mkondo wake.
Ikumbukwe kuwa, katikati ya mwezi Disemba 2024, Jean-Pierre Lacroix, mkuu wa mpango wa amani wa Umoja wa Mataifa alitembelea Jamhuri ya Afrika ya Kati na kukutana na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Felix Moloua ambapo viongozi hao wawili walijadiliana hali ya hivi sasa ya nchi hiyo na hatua muhimu zinazohitajika kwa ajili ya kuboresha mchakato wa kurejesha amani ya kudumu.