Vipaumbele vya Afrika wakati wa uenyekiti wa Afrika Kusini ndani ya G20
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i124654-vipaumbele_vya_afrika_wakati_wa_uenyekiti_wa_afrika_kusini_ndani_ya_g20
Wataalamu na watunga sera waliohudhuria mkutano kuhusu vipaumbele vya Afŕika wakati wa Urais wa Afrika Kusini wa Kundi G20 wamesisitizia haja ya kuyapa kipaumbele mageuzi muhimu ambayo yatasaidia ustawi na maendeleo ya Afŕika na kutumiwa vizuri utajiri mkubwa wa rasilimali wa bara hilo.
(last modified 2025-04-02T00:05:55+00:00 )
Apr 02, 2025 00:05 UTC
  • Vipaumbele vya Afrika wakati wa uenyekiti wa Afrika Kusini ndani ya G20

Wataalamu na watunga sera waliohudhuria mkutano kuhusu vipaumbele vya Afŕika wakati wa Urais wa Afrika Kusini wa Kundi G20 wamesisitizia haja ya kuyapa kipaumbele mageuzi muhimu ambayo yatasaidia ustawi na maendeleo ya Afŕika na kutumiwa vizuri utajiri mkubwa wa rasilimali wa bara hilo.

Wiki hii, Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) Idara ya Maendeleo ya Kiuchumi, Utalii, Biashara, Viwanda na Madini, iliandaa mkutano maalumu mjini Addis Ababa Ethiopia chini ya kaulimbiu ya "Muungano wa Afrika na Afrika Kusini katika G20: Kutetea Ufanisi wa Vipaumbele vya Afrika." Wataalamu na watunga sera katika mkutano huo walitoa mapendekezo yanayotekelezeka kuhusu jinsi AU na bara zima la Afrika linavyoweza kutumia fursa ya urais wa G20 wa Afrika Kusini kufanikisha vipaumbele vya Afrika. Mkutano huo pia ulijadili nafasi ya AU ndani ya G20 kutokana na kwamba huu ni mwaka wa kwanza wa umoja huo kama mwanachama kamili wa G20. Afrika Kusini ilichukua urais wa G20 tarehe 1 Disemba 2024 na itakuwa mwenyeji wa Mkutano wa Viongozi wa G20 mwezi Novemba mwaka huu.

Akihutubia mkutano huo, Patrick Ndzana Olomo, mkuu wa sera za uchumi na maendeleo endelevu katika idara ya Kamisheni ya AU ametaja baadhi ya changamoto zinazokabili uchumi wa Afrika hivi sasa, ikiwa ni pamoja na athari mbaya za mabadiliko ya hali ya hewa, mtikisiko wa uchumi wa dunia, mivutano ya kijiografia na ukosefu wa usalama na athari za mwelekeo wa soko la kimataifa. Olomo amesisitizia msimamo wa pamoja wa Afrika katika kuunga mkono mageuzi ya kudhibitiwa miamala ya fedha duniani ili miamala hiyo ifanyike kiuadilifu na kwa mfumo mzuri usio na ubaguzi wala wa kutangulizwa mbele baadhi ya nchi na kubaguliwa na kukandamizwa nyingine. Pia amesisitizia haja ya kuchukuliwa hatua za haraka za kutenga fedha za kushughulikia hali ya hewa ili kuhakikisha kunakuwa na uwazi, kunatendwa haki na kuna ushirikishwaji wa kiuadilifu. Akibainisha haja muhimu ya kuimarishwa uratibu wa bara zima la Afrika baina ya AU na wanachama wake, Olomo amegusia hatua muhimu zinazopaswa kuchukuliwa wakati wa urais wa G20 wa Afrika Kusini, ikiwa ni pamoja na kupigania kuainishwa na kutekelezwa vipaumbele muhimu zaidi kwa Afrika kama vile kuleta mageuzi ya kimuundo barani humo katika sekta mbalimbali za maendeleo.

 

Kwa upande wake, Hanan Morsy, naibu katibu mtendaji na mwanauchumi mkuu katika Kamisheni ya Tume ya Umoja wa Mataifa ya Uchumi wa Afrika amesema kuwa, bara la Afrika linahitaji kutumia kikamilifu fursa iliyopatikana hivi sasa ya urais wa G20 wa Afrika Kusini kuendeleza msimamo wa pamoja wa bara hilo katika jukwaa la kimataifa. Alisema urais wa G20 wa Afrika Kusini ni fursa muhimu na ya kipekee kwa Afrika kuweka ajenda ya kufanikisha vipaumbele muhimu kama vile mageuzi ya benki za maendeleo za kimataifa na udhibiti wa miamala ya fedha duniani.

Wataalamu wa mambo wanasema kuwa, kuna masuala mengi muhimu yanayolihusu bara la Afrika na dunia kwa ujumla kama vile kukabiliana na uchafuzi wa hali ya hewa unakofanywa na madola makubwa ya viwanda, kuimarisha miundombinu ya umma ya kidijitali, kustawisha mifumo ya huduma za afya na kuwa na maendeleo endelevu.

Wataalamu hao wanasema: Miongoni mwa vipaumbele vya Umoja wa Afrika hasa baada ya kukubaliwa kuwa mwanachama wa G20 mwaka 2023 ni kuhakikisha bara la Afrika linashirikishwa zaidi katika maamuzi muhimu duniani. Lakini pia Umoja wa Afrika umejiwekea malengo ya ustawi na maendeleo ya miaka 50 yaani Ajenda ya mwaka 2063. Malengo hayo hayawezi kufikiwa bila ya kuanishiwa vipaumbele ikiwa ni pamoja na kuhakikisha bara la Afrika linapigania mageuzi katika taasisi za fedha za kimataifa, kuongeza pato la kilimo, sekta ambayo ndiyo uti wa mgogo wa uchumi na maendelea, kuwa na nishati ya uhakika, kukuza biashara na uwekezaji kupitia Eneo la Biashara Huru la Bara la Afrika, kupambana na ubadhirifu wa mali za umma na kujiwekea mikakati mizuri ya miundombinu ya kuweza kukabiliana vizuri na majanga mbalimbali yanayotokea barani Afrika na kukata minyororo ya madola ya kikoloni.

Lakini pia, bara la Afrika lina utajiri mkubwa sana wa maliasili hasa madini. Utajiri huo lazima utumike kuhakikisha unawanufaisha wananchi wa nchi za Afrika. Bila ya shaka ni kwa sababu hiyo pia ndio maana wiki Umoja wa Afrika (AU) ulitoa mwito kwa nchi za Afrika kutumia rasilimali kubwa ya madini ya bara hilo kuleta maendeleo endelevu, ujenzi wa viwanda na mageuzi ya kiuchumi barani humo. Hivyo bila ya shaka ni miongoni mwa vipaumbele vingine vinavyoweza kutumiwa na nchi za Afrika kulinufaisha bara hilo wakati huu wa uenyekiti wa G20 wa Afrika Kusini.