Shirika la Msalaba Mwekundu lakanusha kuhusika na ndege iliyoshambuliwa DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i124794-shirika_la_msalaba_mwekundu_lakanusha_kuhusika_na_ndege_iliyoshambuliwa_drc
Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) imekanusha kuhusika kivyovyote vile na ndege ya misaada ya kibinadamu iliyoshambuliwa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na kusababisha kifo cha mtu mmoja.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Apr 05, 2025 05:33 UTC
  • Shirika la Msalaba Mwekundu lakanusha kuhusika na ndege iliyoshambuliwa DRC

Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) imekanusha kuhusika kivyovyote vile na ndege ya misaada ya kibinadamu iliyoshambuliwa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na kusababisha kifo cha mtu mmoja.

Katika taarifa yake ya jana Ijumaa, ICRC imefafanua kwamba si ndege yake wala wafanyakazi wake waliohusika katika ndege hiyo ya kukodi iliyoshambuliwa wakati ilipokaribia Uwanja wa Ndege wa Kavumba huko Bukavu, makao makuu ya jimbo la Kivu Kusini.

“Shirika letu halina taarifa zozote kuhusu tukio hilo hivyo haliwezi kusema chochote," imesema taaarifa hiyo na kuongeza kuwa: "ICRC inaendelea na kazi yake ya misaada ya kibinadamu na kusaidia watu walioathiriwa na mapigano ya silaha nchini DRC, ikiwa ni pamoja na wale ambao wamekimbilia nchi jirani."

Kauli hiyo imekuja baada ya Chris Magezi, msemaji wa jeshi la Uganda, kusema Jumatatu kwamba ICRC imepata kandarasi ya Kituo cha Mafunzo ya Usafiri wa Anga cha Ocean Heights nchini Uganda ili kuwahamisha wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu waliokuwa wamekwama kwenye mapigano ya silaha katika jimbo la Kivu Kusini. Kwa mujibu wa Magezi, ndege hiyo ni ya shirika la Cessna Caravan iliyoruka kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe Uganda kuelekea Uwanja wa Kazimu.

Magezi amesema: "Ripoti zinaonyesha kuwa mtu mmoja kwenye ndege hiyo alipigwa risasi na kufariki dunia. Serikali ya Uganda, kupitia njia husika za kidiplomasia, inafuatilia suala hili." Amesema hayo sambamba na kukana kuhusika Jeshi la Wananchi wa Uganda katika tukio hilo.

Mwezi Februari mwaka huu waasi wa March 23 waliteka Uwanja wa Ndege wa Kavumba, ulioko umbali wa takriban kilomita 30 kutoka Bukavu. Uwanja huo wa ndege ni kituo muhimu sana cha ndege za masuala ya kibinadamu na za kijeshi.