Umoja wa Afrika wamemteua Rais wa Togo kupatanisha mgogoro wa DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i124836-umoja_wa_afrika_wamemteua_rais_wa_togo_kupatanisha_mgogoro_wa_drc
Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), Joao Lourenco, amemteua Rais wa Togo, Faure Gnassingbe, kuwa mpatanishi kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Rwanda, na waasi wa M23.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Apr 06, 2025 09:38 UTC
  • Umoja wa Afrika wamemteua Rais wa Togo kupatanisha mgogoro wa DRC

Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), Joao Lourenco, amemteua Rais wa Togo, Faure Gnassingbe, kuwa mpatanishi kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Rwanda, na waasi wa M23.

Ofisi ya Lourenco imetangaza kuwa mashauriano ya awali na Gnassingbe yamekuwa na matokeo chanya na uteuzi huo unatazamiwa kuthibitishwa rasmi na viongozi wa Afrika.

Lourenco, ambaye ni Rais wa Angola, "amegusia hali mbaya ya binadamu inayoendelea Mashariki mwa DRC, huku akiashiria mateso makubwa ya raia na athari zake mbaya kwa amani ya kanda."

Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Mahmoud Ali Youssouf, naye amesisitiza haja ya kuwepo mpango wa kina wa kufanikisha upatanishi, na kuongeza kuwa tume itafuata utaratibu wa kuidhinisha uteuzi wa Rais wa Togo.

Mara tu atakapoidhinishwa, Gnassingbe ataongoza jopo la wapatanishi wengine watano walioteuliwa hivi karibuni na wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Jopo hilo la kieneo linajumuisha Rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanji,  na marais wengine wa zamani ambao Uhuru Kenyatta wa Kenya, Kgalema Motlanthe waAfrika Kusini , Sahle-Work Zewde waEthiopia), na Catherine Samba-Panza wa Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Katika miezi ya hivi karibuni waasi wa M23 wameyateka maeneo mengi ya majimbo ya Kivu Kaskazini na Kusini  tangu washadidishe hujuma zao dhidi ya maeneo mbalimbali mashariki mwa DRC mwaka jana.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na baadhi ya nchi zinaituhumu Rwanda kuwa inawaunga mkono waasi wa M23, hata hivyo Kigali, inakanusha madai hayo.