Wakenya kwenye mitandao ya kijamii: Bunge limekuwa paradiso ya walafi
-
Bunge la Kenya
Baadhi ya raia wa Kenya wanaotumia mitandao ya kijamii wameeleza kukasirishwa na hatua ya wabunge na maseneta ya kujiongezea posho za usafiri kupitia marekebisho ya marupurupu kwa kima cha jumula cha Sh bilioni 4.4.
Wakenya hao wamekosoa vikali hatua hiyo ya wabunge na maseneta kujiongea karupurupu huku sehemu kubwa ya jamiii ikisumbuliwa na hali mbaya ya uchumi.
Kuanzia Aprili 1, 2025, Wabunge wanatarajiwa kupokea nyongeza ya posho ya Sh 366,011 kwa mwezi kama sehemu ya malipo mapya ya kusafiri kwa magari yao kila mwezi. Hatua hii imeibua hasira mitandaoni huku Wakenya wakijiuliza ni vigezo gani vilivyotumika kuidhinisha ongezeko hilo katika taifa linalopambana na matatizo ya kiuchumi.
Baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii wamesema, hatua hiyo inalidhihirisha Bunge kama paradiso la walaghai wanaojijali huku raia wakiendelea kuteseka kutokana na gharama ya juu ya maisha. Raia hao wamewataja wabunge kama matapeli wakuu wanaotumia mamlaka yao ya uwakilishi kujinufaisha.
Vyombo vya habari vya Kenya vimeripoti leo kuwa, katika kile kinachoonekana kuwa sehemu ya mchakato wa kisiasa ulioendeshwa kimya kimya, hakuna taasisi ya umma iliyojitokeza kueleza kilichoendelea. Na zaidi ni kwamba, wananchi waliokuwa na uelewa finyu au waliokata tamaa wametetea hatua hiyo wakisema marekebisho hayo si nyongeza ya mishahara.
Hata hivyo hali ilikuwa tofauti kwa baadhi ya Wakenya hasa katika mitandao ya kijami.
@Biko_Mkenya ameandika katika mtandao wa kijamii wa X kwamba: “Wabunge wetu wanaongeza posho huku bei ya unga ikipanda kila wiki. Hii Kenya si ya wananchi tena, ni paradiso ya matapeli wa kisiasa!.”
Maureen Atieno ameandika katika ukurasa wake wa Facebook kwamba: “Sisi wa Ugunja hatujui hata mbunge wetu ni nani kwa sasa, lakini maisha yanaendelea tu. Hawa watu hawafai.”
Wachambuzi wa siasa na wataalamu wa mambo pia wanakubaliana na raia kuwa katika mfumo wa ugatuzi, viti vya Wawakilishi wa Wadi, Mbunge, Seneta na Mwakilishi wa Wanawake zimepoteza maana na umuhimu wake nchini.
Mchambuzi wa siasa Joseph Kiilu anasema: “Hali imekuwa mbaya chini ya utawala wa sasa, viti hivi havina maana kwa mwananchi wa kawaida. Hizi ni nyadhifa ambazo zimegeuzwa kuwa ngazi za kujitajirisha, sio kutetea raia na kufanya serikali iwajibike.”