Ubalozi wa Marekani wazingirwa na waaandamanaji nchini Mauritania
Wananchi wenye hasira wa Mauritania wamefanya maandamano makubwa na kuuzingira ubalozi wa Marekani mjini Nouakchott wakilaani jinai za Israel katika Ukanda wa Ghaza na kushiriki kikamilifu Washington katika jinai hizo.
Mashirika mbalimbali ya habari yameripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, jana Jumatatu wananchi wa Mauritania waliitikia vilivyo mwito wa kimataifa wa kushikamana na wananchi wa Ukanda wa Ghaza.
Mamia ya waandamanaji wamekusanyika mbele ya ubalozi wa Marekani mjini Nouakchott wakilaani jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina na kuuzingira ubalozi wa Marekani kuonesha hasira zao kutokana na kushiriki kikamilifu Washington katika jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Waandamanaji hao wamepiga nara za kuulaani utawala wa Kizayuni na kutoa mwito wa kususiwa nchi zote zinazouunga mkono utawala huo ghasibu.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Mauritania, makundi mbalimbali ya wananchi wa nchi hiyo, wakiwemo wafanyabiashara, wanafunzi wa vyuo vikuu na watu wengine wameitikia vyema mwito wa kimataifa wa mshikamano na Ghaza kwa kushirikia kwa maelfu katika maandamano hayo.
Wananchi wa Mauritania waliandamana pia mbele ya ubalozi wa Marekani mjini Nouakchott Jumamosi jioni kupinga mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel katika Ukanda wa Ghaza.
Washiriki wa maandamano hayo walitangaza hadharani kwamba Marekani ndiyo inayobeba dhima yote ya kuendelea mauaji ya umati ya Israel huko Ghaza na kutoa mwito wa kukatishwa uhusiano wa kidiplomasia na Washington.