Idadi ya waliofariki dunia kwa mafuriko DRC yaongezeka, vita vinaendelea
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i124894-idadi_ya_waliofariki_dunia_kwa_mafuriko_drc_yaongezeka_vita_vinaendelea
Mbali na majanga ya ukosefu wa amani na vita baina ya makundi hasimu, majanga ya kimaumbile yanaikumba pia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Watu wasiopungua 33 wamethibitishwa kufarikidunia kufuatia mvua kubwa iliyonyesha Kinshasa, mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wakati juzi Jumapili idadi hiyo ilikuwa ni watu 22.
(last modified 2025-04-07T22:58:55+00:00 )
Apr 07, 2025 22:58 UTC
  • Idadi ya waliofariki dunia kwa mafuriko DRC yaongezeka, vita vinaendelea

Mbali na majanga ya ukosefu wa amani na vita baina ya makundi hasimu, majanga ya kimaumbile yanaikumba pia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Watu wasiopungua 33 wamethibitishwa kufarikidunia kufuatia mvua kubwa iliyonyesha Kinshasa, mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wakati juzi Jumapili idadi hiyo ilikuwa ni watu 22.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Ndani na Usalama wa DRC, Jacquemain Shabani amethibitisha habari hiyo na kuongeza kuwa, mvua kubwa iliyonyesha mfululizo usiku wa kuamkia Ijumaa na kuendelea hadi Jumamosi, imesababisha uharibifu mkubwa katika wilaya kadhaa za mji mkuu Kinshasa, na kuacha watu wengi kupoteza maisha na kujeruhiwa na nyumba nyingine kuharibiwa.

Serikali ya DRC imeanzisha kitengo maalumu cha kudhibiti mgogoro kinachoendeshwa na jeshi, wizara kadhaa na serikali ya mkoa wa Kinshasa ili kuendesha zoezi la uokoaji na kupeleka mahitaji ya dharura.

Mafuriko hayo yameharibu miundombinu mingi ya jiji hilo, kukata barabara kuu na kusababisha kukatika umeme na maji katika jiji zima.

Wizara ya Uchukuzi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imeripoti kutokea matatizo makubwa katika njia za kwenda na kurudi kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa N'djili kiasi kwamba serikali imeamua kutumia kivuko cha dharara cha majili ili kuwasaidia wasafiri waliokwama.

Wataalamu wa hali ya hewa wametabiri kuendelea kunyesha mvua kubwa katika siku zijazo, na kuzua hofu ya kutokea uharibifu zaidi katika jiji la Kinshasha lenye watu milioni 17.

Kwa kawaida msimu wa mvua Jamhuri ya Kidemokrsia ya Congo (DRC) huanza Novemba hadi Mei.