Kihausa, lugha ya kitaifa ya Niger baada ya Kifaransa kupunguzwa hadhi
Katika hatua ya kijasiri ya kuelekea kwenye uhuru kamili na kuondoa mabaki ya ukoloni, Niger imetangaza Kihausa kuwa lugha ya kitaifa huku lugha ya Kifaransa ikiwa imeshushwa hadhi.
Tangazo hilo ni sehemu ya Mkataba wa Mageuzi (Refoundation Charter) uliopitishwa hivi karibuni na kuchapishwa katika Jarida Rasmi la Serikali ya Niger, kabla ya kusambazwa kwa kiwango kikubwa mtandaoni na waandishi wa habari pamoja na watumiaji wa mitandao ya kijamii.
Hatua hiyo inaashiria mabadiliko makubwa katika utambulisho wa taifa na mfumo wa utawala, ikiwa ni matokeo ya miezi kadhaa ya misukosuko ya kisiasa na kuongezeka hisia za kupinga ukoloni.
Lugha ya Kifaransa imepoteza hadhi yake kama lugha rasmi nchini Niger baada ya nchi tatu za Muungano wa Sahel ambazo ni Burkina Faso, Mali na Niger kujiondoa katika Shirika la Kimataifa la Nchi Zinazozungumza Kifaransa (OIF).
Dhamira iliyotangazwa ya OIF ni kukuza lugha ya Kifaransa, kusaidia amani na demokrasia, na kukuza elimu na maendeleo katika nchi zinazozungumza Kifaransa duniani, nyingi ambazo zilikuwa makoloni ya zamani ya Ufaransa .
Nchi hizo tatu za Sahel zinasema OIF imepoteza mwelekeo wake wa awali wa kukuza ushirikiano wa kitamaduni na kiufundi, na kuwa chombo chenye upendeleo cha "ghiliba ya kisiasa."
Hivi karibuni Waziri wa Mambo ya Nje wa Mali, Abdoulaye Diop, alisema kuwa Muungano wa Mataifa ya Sahel (AES) umebadili kabisa mlingano wa nguvu za kimkakati kwa madola ya kikoloni ambayo yanataka kuendelea kutawala nchi hizo.
Diop alisema: "Hakika kuna changamoto kubwa…zinazotokana na nguvu za zamani za kikoloni au mataifa ya Magharibi, na pia kutoka kwa wahusika wa kikanda wanaotaka kutawala au kuongoza mataifa yetu."
Kwa sasa, Muungano huo unafanya mabadiliko makubwa ya kistratejia ya kimataifa, ikiwemo kujiondoa katika Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS).
AES pia imetangaza mpango wa kuunda jeshi la pamoja la wanajeshi 5,000 kupambana na tishio la ugaidi katika eneo hilo. Hatua nyingine ni pamoja na uzinduzi wa pasipoti ya pamoja na televisheni ya mtandaoni itakayosaidia kupambana na upotoshaji wa habari.