Misri: Tunatumai mazungumzo ya Iran na Marekani yatasaidia kupunguza mivutano
(last modified Sun, 13 Apr 2025 10:34:11 GMT )
Apr 13, 2025 10:34 UTC
  • Misri: Tunatumai mazungumzo ya Iran na Marekani yatasaidia kupunguza mivutano

Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri imetangaza kuwa inatarajiwa mazungumzo kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Marekani yataanzisha awamu mpya itakayosaidia kuimarisha amani na kupunguza mivutano katika eneo la Magharibi mwa Asia kwa ujumla hususan Ukanda wa Gaza.

Shirika la habari la al Sharq al Ausat limeripoti kuwa, Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri imetoa taarifa na kukaribisha duru ya kwanza ya mazungumzo kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Marekani kuhusu miradi ya nyuklia ya Tehran na kupongeza mchango wa Oman katika kuunga mkono njia za kisiasa na za amani kwa kuzingatia changamoto kubwa zinazoikabili kanda hii na hivyo kuondoa hofu ya vita vya pande zote katika eneo la Asia Magharibi. 

Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri inasisitiza kuwa inaunga mkono kikamilifu juhudi za Oman na nyingine zote zenye lengo la kupata ufumbuzi wa kisiasa kupitia mazungumzo. 

"Misri imekuwa ikiunga mkono njia hii kwa muda mrefu kwa sababu Cairo inaamini kikamilifu kuwa njia za kijeshi haziwezi kutatua migogoro na kwamba sera za kuzidisha mivutano na mapigano hazina manufaa yoyote ghairi ya kuchochea hali ya mgogoro", imeongeza taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri. 

Duru ya kwanza ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani ilifanyika mjini Muscat jana Jumamosi, Aprili 12  kwa kusimamiwa na Oman.