Watu 7 wauawa katika shambulizi kaskazini-kati mwa Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i125238-watu_7_wauawa_katika_shambulizi_kaskazini_kati_mwa_nigeria
Wafugaji waliokuwa na silaha jana Jumanne waliishambulia jamii ya Otobi katika Jimbo la Benue kaskazini-kati mwa Nigeria, siku moja baada ya kundi lililokuwa na silaha kuwaua watu 51 katika Jimbo la Plateau.
(last modified 2025-04-16T04:27:05+00:00 )
Apr 16, 2025 04:27 UTC
  • Watu 7 wauawa katika shambulizi kaskazini-kati mwa Nigeria

Wafugaji waliokuwa na silaha jana Jumanne waliishambulia jamii ya Otobi katika Jimbo la Benue kaskazini-kati mwa Nigeria, siku moja baada ya kundi lililokuwa na silaha kuwaua watu 51 katika Jimbo la Plateau.

Shambulio hilo katika wilaya ya Akpa katika eneo la serikali ya mtaa ya Otukpo, limesababisha vifo vya watu saba na wengine zaidi ya 20 kujeruhiwa, huku nyumba nyingi zikiteketezwa kwa moto.

Kennedy Angbo, mbunge anayewakilisha Eneo Bunge la Otukpo-Akpa katika Bunge la Jimbo la Benue ameeleza kuwa shambulio hilo lilitokea mwendo wa saa  kumi na moja na nusu asubuhi jana Jumanne na kuendelea kwa masaa mawili.

"Tunahitaji msaada, kwani watu wetu wanauawa bila huruma,” amesema Angbo kwa njia ya simu, na kuongeza kuwa mamia ya watu wameikimbia jamii hiyo.

Jamii ya watu wa Otobi katika mwezi huu wa Aprili imeshambuliwa mara tatu na watu wenye silaha. 

Mgogoro kati ya wakulima na wafugaji, ambao umesababisha maelfu ya watu kupoteza maisha, ni kati ya  changamoto kubwa zaidi za usalama nchini Nigeria katika miaka ya hivi karibuni.

Mgogoro huo, ambao kimsingi ni tatizo la udhibiti wa rasilimali kati ya wakulima na wafugaji nchini Nigeria, unazidisha kasi ya mgawanyiko wa kikabila, kikanda na kidini.