Rais Pezeshkian asema Iran itatekeleza mapatano ikiwa Marekani itafanya hivyo
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i139540-rais_pezeshkian_asema_iran_itatekeleza_mapatano_ikiwa_marekani_itafanya_hivyo
Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, amesisitiza kuwa makubaliano yoyote kati ya Iran na Marekani lazima yajikite katika heshima ya pande zote na ahadi za pamoja, na si kwa kutumia vitisho au shinikizo la upande mmoja.
(last modified 2026-06-30T11:32:19+00:00 )
Jun 30, 2026 11:31 UTC
  • Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian
    Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian

Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, amesisitiza kuwa makubaliano yoyote kati ya Iran na Marekani lazima yajikite katika heshima ya pande zote na ahadi za pamoja, na si kwa kutumia vitisho au shinikizo la upande mmoja.

Katika chapisho lake kwenye mtandao wa X usiku wa Jumatatu, Rais Pezeshkian ameandika hivi: “Mapatano ni njia ya pande mbili. Ikiwa upande wa Marekani utazingatia makubaliano, sisi pia tutatekeleza ahadi zetu.”

Aliongeza kuwa: “Msimamo wetu dhidi ya vitisho vya kijeshi visivyo na msingi na shutuma zisizo na mashiko ni kutegemea busara na utu katika kufanya maamuzi, huku tukijitayarisha kutetea maslahi yetu kwa ujasiri na bila hofu wakati ukifika wa kuchukua hatua.”

Kauli hizi zinakuja wakati pande zote mbili zikijitahidi kutekeleza Mkataba wa Maelewano (MoU) uliopatanishwa na Pakistan na Qatar, ambao unalenga kukomesha mzunguko wa hivi karibuni wa uchokozi wa Marekani na utawala wa Kizayuni, na kupunguza mivutano katika kanda hii.

Iran imeendelea kuonyesha utayari wa diplomasia ya dhati inayozingatia haki na usawa, huku ikikataa aina yoyote ya mashinikizo au ahadi hewa.

Maafisa wa Iran wamesisitiza mara kwa mara kwamba ingawa Jamhuri ya Kiislamu inatafuta suluhu za amani kupitia mazungumzo, bado iko tayari kikamilifu kulinda mamlaka yake na heshima ya taifa kwa nguvu na azimio thabiti.

Akisisitiza msimamo huo, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Esmaeil Baghaei, ametangaza Jumatatu kuwa mazungumzo ya kiufundi na Marekani yataanza tu pindi masharti muhimu ya mkataba wa maelewano wa pointi 14 yatakapokuwa yametekelezwa kikamilifu.