Polisi wa Afrika Kusini wakabiliana na waandamanaji wanaopinga wageni
-
Waandamanaji Afrika Kusini wanaopinga raia wa kigeni nchini humo
Mamlaka nchini Afrika Kusini zimeimarisha ulinzi kwa kupeleka vikosi vya polisi katika miji mikuu ya nchi hiyo, kufuatia wimbi la maandamano dhidi ya raia wa kigeni wasio na nyaraka rasmi za ukaazi.
Makundi ya wananchi wanaoipinga hatua ya wageni kushiriki katika shughuli za kiuchumi nchini humo, yalikuwa yametoa makataa ya hadi leo kwa wahamiaji hao waondoke nchini kwa hiari, la sivyo waondolewe kwa nguvu.
Maafisa wa usalama wameonekana wakishika doria katika kitovu cha biashara jijini Johannesburg, ambapo wafanyabiashara wengi wamechagua kusitisha shughuli zao kwa muda. Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya ndani askari wa Jeshi la Afrika Kusini wameonekana wailinda doria katika maeneo kadhaa ya mikakati.
Katika jiji la Durban, maandamano yameshuhudiwa yakihusisha zaidi ya watu 5,000 waliokuwa wamejihami kwa viboko na rungu za kitamaduni za Kizulu. Hali ya taharuki ilitanda ghafla wakati kundi hilo lilipoanza kusonga mbele katika mitaa ya jiji.
Ingawa baadhi ya maduka katika maeneo ya biashara yamefungwa, mengine yamebaki wazi chini ya ulinzi mkali. Katika mtaa wa Hillbrow, jijini Johannesburg, visa vya waandamanaji kurusha mawe vimeripotiwa.
Kupitia taarifa rasmi iliyotolewa mchana wa Jumanne, Wizara ya Polisi imethibitisha kufanyika kwa ukamataji wa baadhi ya wahusika wa ghasia hizo, ingawa haikuweka wazi idadi kamili wala maeneo mahususi ya matukio hayo.
Upelekaji wa vikosi hivyo unaonekana kama hatua ya dharura ya kuzuia uporaji wa mali na ghasia za umati, ili kuepuka kadhia kama ile ya mwaka 2008 iliyosababisha vifo vya watu 62. Aidha, tukio hili linakumbusha machafuko makubwa ya Julai 2021, yaliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 350, ambayo yalikuwa mabaya zaidi kuwahi kushuhudiwa tangu kumalizika kwa mfumo wa ubaguzi wa rangi (Apartheid).
Kwa kipindi cha wiki kadhaa za mwezi Mei na Juni, makundi ya wanaume wakiwa na silaha za jadi na wakiimba kauli mbiu ya “abahambe” (neno la Kizulu na Kixhosa lenye maana ya “lazima waondoke”), yamekuwa yakipita duka kwa duka, wakiwahoji na wakati mwingine kuwashambulia wahamiaji katika miji ya Johannesburg na Durban. Kwa mujibu wa taarifa kutoka nchi jirani ya Msumbiji, raia wake watano walipoteza maisha kufuatia mashambulizi hayo.
Wahamiaji wanakadiriwa kufikia asilimia 4 pekee ya wakazi milioni 62 wa Afrika Kusini, licha ya dhana potofu zinazodai kuwa idadi yao inafikia milioni 15 hadi 20. Wahamiaji wengi hujikita katika sekta isiyo rasmi, wakikimbia msukosuko wa kiuchumi katika nchi zao ili kutafuta fursa katika moja ya mataifa yenye uchumi mkubwa zaidi barani Afrika.
Serikali za mataifa kadhaa, ikiwemo Nigeria, Kenya, Ghana, Malawi, na Uganda, zimeanza utaratibu wa kuwarejesha makwao raia wake kabla ya makataa hayo kumalizika, huku wengine bado wakiwa wamekwama katika mazingira magumu. Picha zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha makundi ya raia wa Malawi wakipiga kambi katika baridi nje ya ubalozi wao jijini Johannesburg, wakisubiri kukamilishiwa taratibu za kusafirishwa nje ya nchi.