Umoja wa Mataifa: Ebola kuigharimu Afrika dola Bilioni 3.6
-
Ebola kuigharimu Afrika dola Bilioni 3.6
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, mlipuko wa virusi vya Ebola huenda ukaligharimu bara la Afrika kiasi cha dola za Marekani bilioni 3.6 pamoja na maelfu ya ajira na pengine kusababisha mzozo wa kimaendeleo kwenye bara hilo.
Ripoti ya tathmini iliyofanywa na shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu maendeleo, inaeleza kuwa, madhara ya janga hili yanakwenda nje ya sekta ya afya na lisipodhibitiwa hasara itakuwa kubwa zaidi.
Ikiwa mlipuko huu unaohusishwa na virusi vya Bundibugyo, hautadhibitiwa ndani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo utagharimu bilioni moja ya mapato ya kitaifa ya DRC, ripoti imeonesha.
Wataalamu wanasema licha ya kuwa nchi ya Uganda imeripoti idadi ndogo ya wagonjwa wa Ebola, lakini kuna uwezekano mkubwa uugonjwa huo ukaenea kwenye nchi jirani ya Sudan Kusini na nchi nyingine katika kanda hiyo.
Aidha ripoti imeongeza kuwa nchini Jamhuri ya Kidemokrasaia ya Congo watu zaidi ya milioni moja watatumbukia kwenye umaskini hata kama janga hili litadhibitiwa.
Kwa mujibu wa shirika la maendeleo la umoja wa Mataifa, UNDP, mikakati ya kudhibiti msambao imeathiri biashara, usafiri na shughuli za kiuchumi na kuweka shinikizo kwenye maisha ya wengi nchini DRC na nchi jirani.
Wakati huo huo, Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wamejulishwa kuwa kuongezeka kwa mapigano, kuzorota kwa hali ya kibinadamu na mlipuko mpya wa Ebola kunazidi kuongeza mateso kwa wananchi wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, (DRC) licha ya juhudi za kikanda za kuleta amani kuendelea kupata mafanikio.