Wananchi wa Morocco wafanya maandamano 105 kuiunga mkono Gaza
(last modified Sat, 19 Apr 2025 06:05:54 GMT )
Apr 19, 2025 06:05 UTC
  • Wananchi wa Morocco wafanya maandamano 105 kuiunga mkono Gaza

Televisheni ya al Jazeera yenye makao yake nchini Qatar imetangaza kuwa wananchi wa Morocco wamefanya maandamano 105 katika miji 58 ya nchi hiyo wakitangaza mshikamano wao na kuwaunga mkono watu madhulumu wa Ukanda wa Gaza na kulaani vita vya mauaji ya kimbari vya utawala wa Kizayuni wa Israel katika eneo hilo.

Televisheni ya al Jazeera imeongeza kuwa, Wananchi wa Morocco wameshiriki katika maandamano 105 yaliyoshuhudiwa katika miji 58 ya nchi hiyo kwa lengo la kuwaunga mkono wananchi madhulumu wa Ukanda wa Gaza na kulaani mashambulizi ya jeshi la utawala wa Kizayuni. 

Katika maandamano hayo, wananchi wa Morocco pia wametangaza kupinga kutia nanga meli zinazoelekea Israel katika bandari za nchi hiyo.

Wakati huo huo, Redio ya Sauti ya Morocco imeripoti kuwa mamia ya wananchi jana Ijumaa waliandamana karibu na bandari ya  Dar El Yaba (Casablanca) wakipinga kutia nanga kwa meli ya Nexoe Maersk, inayoshukiwa kusafirisha vipuri vya ndege aina ya F-35 hadi Israel (huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu).

Wamorocco wametaka kupigwa marufuku kutia nanga meli kubwa za kampuni ya usafrishaji wa baharini ya Maerks Line katika bandari za Morocco.