Wahajiri wa Kiafrika waaga dunia kwa baridi mpaka wa Morocco, Algeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i134338-wahajiri_wa_kiafrika_waaga_dunia_kwa_baridi_mpaka_wa_morocco_algeria
Wahamiaji tisa wa Kiafrika wamepoteza maisha kutokana na baridi kali karibu na mpaka wa Morocco na Algeria.
(last modified 2025-12-15T11:01:34+00:00 )
Dec 15, 2025 11:01 UTC
  • Wahajiri wa Kiafrika waaga dunia kwa baridi mpaka wa Morocco, Algeria

Wahamiaji tisa wa Kiafrika wamepoteza maisha kutokana na baridi kali karibu na mpaka wa Morocco na Algeria.

Miili ya wanaume saba na wanawake wawili ilipatikana huko Ras Asfour, eneo la milimani la Morocco linalojulikana kwa viwango vikali vya baridi, Chama cha Haki za Binadamu cha Morocco kilisema Jumamosi katika taarifa.

"Walikufa kutokana na baridi kali, ambayo miili yao iliyochoka haikuweza kustahimili," imesema taarifa ya chama hicho. Makundi ya haki za binadamu katika nchi hiyo ya Afrika Kaskazini yameliita janga hilo la kusikitisha kuwa ukiukwaji wa haki ya uhuru wa kutembea.

Mmoja wa wahamiaji hao alikuwa raia wa Guinea, duru za habari zimearifu na kuongeza kuwa, wahanga wengine ni raia nchi tofauti za Kusini mwa Jangwa la Sahara barani Afrika, ingawa taarifa maalum kuhusu utambulisho wao bado haijulikani.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Morocco haijatoa maelezo kuhusu uraia wa watu waliopoteza maisha kwenye tukio hilo.

Kila mwaka, maelfu ya wahamiaji wanaotafuta maisha mazuri hujaribu kuingia Ulaya kinyume cha sheria kutoka Afrika Kaskazini; huku njia kuu ikiwa ni kutoka Morocco hadi Uhispania.

Katika hatua nyingine, watu wasiopungua 21 wamefariki dunia kutokana na mafuriko ya ghafla yaliyosababishwa na mvua kubwa katika mkoa wa pwani wa Safi nchini Morocco, yapata kilomita 330 (maili 205) kusini mwa Rabat, mamlaka ya Morocco imesema.
Mafuriko hayo ya jana Jumapili pia yamewajeruhi watu 32. Baadhi yao wamelazwa hospitalini na wengi wao wamesharuhusiwa kuondoka hospitalini, mamlaka imesema katika taarifa.