Jumatano, 12 Novemba, 2025
Leo ni Jumatano tarehe 21 Jamadil Awwal 1447 Hijria sawa na 12 Novemba 2025.
Miaka 1126 iliyopita katika siku kama ya leo sawa na tarehe 21 Mfunguo 8 mwaka 320 Hijria, alizaliwa Abu Ja'far Ahmad bin Ibrahim Qirawani, aliyekuwa mashuhuri kwa jina la Ibn Jazzar.
Msomi huyo wa Morocco alikuwa tabibu, mwanafalsafa na mwanajiografia mashuhuri wa Kiislamu. Ibn Jazzar alikuwa tabibu mwenye moyo wa kujitolea na anayewatakia watu kheri na aliandika kitabu alichokipa jina la "Twibul Fuqaraa” au Tiba ya Watu Maskini."
Mwanafalsafa huyo ameandika vitabu 20. Miongoni mwa vitabu vyake ni Risalatun Fii Ibdalil Adwiya na Zadul Musafir.
Siku kama ya leo miaka 128 iliyopita alizaliwa Ali Isfandiyari mashuhuri kwa jina la Nima Yushij, mwasisi wa mashairi ya kisasa nchini Iran.
Isfandyari alizaliwa katika mojawapo ya vijiji vya mkoa wa Mazandaran kwa jina la Yush huko kaskazini mwa Iran. Malenga huyo baadaye alielekea Tehran na kuanza kujifunza lugha ya Kifaransa. Nima Yushij alianza kutunga mashairi na kubuni mfumo mpya wa mashairi.
Miongoni mwa sifa za mfumo huo wa mashairi mapya ni kueleza masuala ya jamii kwa lugha nyepesi. Kazi muhimu zaidi ya malenga huyo mashuhuri wa Iran ni maarufu kwa jina la "Afsaneh".
Miaka 111 iliyopita katika siku kama ya leo, kulitolewa fatuwa ya Marajii Taqlidi wa Kishia na Maulamaa wakubwa wa Iraq kwa ajili ya kukabiliana na uvamizi wa Uingereza.
Hiyo ilikuwa ni katika kipindi cha kujiri Vita vya Kwanza vya Dunia. Katika zama hizo ardhi ya Iraq ya leo ilikuwa sehemu ya utawala wa Othmania ambapo wanajeshi wake hawakuwa na uwezo wa kulinda ardhi hiyo mbele ya Waingereza.
Licha ya kuwa, Mashia wa Iraq walikuwa wamedhurika kutokana na ubaguzi na udhalimu wa utawala wa Othmania, lakini kutokana na fatuwa ya Maulamaa wao walijitokeza na kukabiliana na uvamizi wa Uingereza.

Katika siku kama ya leo miaka 107 iliyopita yaani Novemba 12 mwaka 1918, utawala wa kifalme ulikomeshwa nchini Austria na kuanza kipindi cha utawala wa Jamhuri baada ya kushindwa utawala wa Austria na Hungary katika Vita vya Kwanza vya Dunia na kutengana nchi hizo mbili.
Mfalme wa mwisho wa Austria, Charles wa Kwanza ambaye alitawazwa kuwa mfalme wa nchi hiyo tarehe 21 Novemba mwaka 1916, alijiuzulu uongozi siku moja tu baada ya kutiwa saini makubaliano ya kusimamisha Vita vya Kwanza vya Dunia hapo tarehe 11 Novemba mwaka 1918 na kuomba hifadhi nchini Uswisi.

Siku kama ya leo miaka 83 iliyopita, vita vya kihistoria vilivyopewa jina la al-Alamein vilimalizika katika mji wenye jina kama hilo huko kaskazini mwa Misri kati ya wanajeshi wa Uingereza na jeshi la Manazi wa Ujerumani.
Vita hivyo vilimalizika baada ya kushindwa jeshi la Ujerumani, japokuwa mapigano kati ya pande hizo mbili yaliendelea katika maeneo mengine ya kaskazini mwa Afrika.
Amani kamili ilipatikana katika maeneo hayo baada ya kushindwa kikamilifu jeshi la Ujerumani wakati wa Vita vya Pili vya Dunia.

Miaka 69 iliyopita katika siku kama ya leo, askari wa utawala haramu wa Israel walifanya mauaji mengine ya umati dhidi ya Wapalestina wasio na hatia katika kambi kubwa ya Wapalestina ya Rafah huko katika Ukanda wa Gaza.
Jinai hiyo ilifanyika siku chache tu baada ya kutangazwa usitishaji vita baina ya Israel, Ufaransa na Uingereza dhidi ya Misri. Hujuma hiyo ya kinyama ilisababisha mauaji ya Wapalestina 110, wakiwemo wanawake na watoto na kujeruhi wengine 1,000.
