Shughuli za chama cha Kabila zasitishwa na serikali ya DRC
Mali za rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Joseph Kabila zimevamiwa na vyombo vya usalama na shughuli za chama chake zimesimamishwa nchi nzima.
Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, imesema imekisimamisha chama cha kisiasa cha rais wa zamani Joseph Kabila, siku chache baada ya kuvamiwa kwa mali zake na vyombo vya usalama.
Wizara ya mambo ya ndani ilitoa taarifa iliyoonesha tarehe ya siku ya Jumamosi, ikisema uamuzi huo umechukuliwa kufuatia harakati za chuki zinazofanywa na Kabila ambaye aliwahi kuwa rais wa taifa hilo kwa miaka 18 hadi mwaka 2019.
Kabila bado ni kiongozi wa chama cha kisiasa cha Peoples Party for Reconstruction and Democracy PPRD. Taarifa hiyo pia iliweka wazi kwamba shughuli zote za chama hicho zimesimamishwa nchi nzima.
Hadi sasa hakuna tamko lililotolewa na PPRD. Rais wa sasa wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo Felix Tshisekedi amemtuhumu Kabila kwamba anaandaa kile alichosema ni ''Uasi '' na anaunga mkono muungano unaojumuisha kundi la M23 ambalo linaendesha vita dhidi ya vikosi vya serikali katika eneo la Mashariki mwa nchi.
Kabila mwenye umri wa miaka 53, aliondoka nchini Kongo kabla ya uchaguzi wa rais mnamo mwaka 2023 kwa mujibu wa msemaji wa familia yake.
Lakini mwanzoni mwa mwezi Aprili, zilitoka taarifa zilizowasilishwa na timu yake zilizosema kwamba rais huyo wa zamani amesema atarejea katika tarehe ambayo haikutajwa,kwasababu nchi iko katika hali ''mbaya''.
Lakini pia zipo taarifa ambazo hazijathibitishwa zinazoonesha kwamba ataingia Kongo,au amekwishaingia katika mji wa Mashariki wa Goma.