Papa wa Misri: Wapalestina wa Gaza wanakabiliwa na dhulma za kuogofya
-
Papa Tawadros II
Papa Tawadros II, Kiongozi wa Kanisa la Kiorthodoksi la Coptic la Misri, amelaani vikali mashambulizi yanayoendelea kufanywa na Israel katika Ukanda wa Gaza na kuyataja kama "moja ya aina mbaya zaidi za dhuluma" dhidi ya Wapalestina.
"Wapalestina wanakabiliwa na aina mbaya zaidi ya dhulma katika maisha yao ya kila siku, huku kukiwa na uharibifu wa nchi yao," Papa Tawadros aliiambia televisheni ya taifa wakati wa sherehe za Pasaka jana Jumapili.
"Misri, kupitia taasisi na vyombo vyake vyote, inapinga kwa sauti moja (Wapalestina) kulazimishwa kuhama au (kuhamishwa) kwa hiari. Kama Rais Abdel Fattah al-Sisi alivyosema, kamwe hatutakuwa sehemu ya dhuluma hii," alisisitiza.
Papa pia amesisitiza juu ya msimamo unaofanana wa Kanisa la Makhufti (Coptic) na Al-Azhar, taasisi kubwa zaidi ya Kiislamu ya Misri, kuhusu mashambulizi ya Israel dhidi ya Wapalestina.
"Tuna maono moja na Imamu Mkuu wa Al-Azhar, Sheikh Ahmed El-Tayyib, kwamba dhamiri ya ulimwengu lazima iamke ili kuwaokoa watu wetu huko Gaza."
Haya yanajiri siku chache baada ya maelfu ya wananchi wa Misri kutoka majimbo mbalimbali kuandamana mjini El-Arish katika Mkoa wa Sinai Kaskazini, wakitangaza kuunga mkono kadhia ya Palestina na kupinga jaribio lolote la kuwafurusha Wapalestina kutoka katika ardhi zao.
Zaidi ya Wapalestina 51,200 wameuawa shahidi huko Gaza katika mashambulizi ya kikatili ya Israel tangu Oktoba 2023, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.