Pandor ahimiza mageuzi ya kimataifa kutekeleza uamuzi wa ICJ kuhusu Gaza
(last modified Wed, 23 Apr 2025 02:12:10 GMT )
Apr 23, 2025 02:12 UTC
  • Pandor ahimiza mageuzi ya kimataifa kutekeleza uamuzi wa ICJ kuhusu Gaza

Naledi Pandor Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini amesema kuwa kushindwa kusitishwa mashambulizi na mauaji ya kimbari ya Israel katika Ukanda wa Gaza kumefichua mapungufu ya mifumo ya kisheria ya kimataifa na kuibua upya wito kuhusu udharura wa kufanyika mageuzi katika Umoja wa Mataifa.

Pandor (71) alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini wakati nchi hiyo ilipowasilisha kesi ya mauaji ya kimbari dhidi ya Israel katika Mahakama ya ICJ mwezi Disemba 2023. 

Baada ya hatua hiyo ya Afrika Kusini, mahakama ya ICJ iliiagiza Israel kuchukua hatua zote za kuzuia vitendo vya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza, na kuhakikisha inaruhusu misaada ya kibinadamu na huduma nyingine muhimu kuingia Gaza. 

Akizungumza katika mahojiano mjini Istanbul, Uturuki, waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Afrika Kusini amesema: "Hatuwezi kuwa na mfumo dhaifu wa dunia huku watu wanauawa kiholela."

Marekani inaiunga mkono Israel katika mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza na imetumia kura yake ya veto mara kadhaa kuzuia kuchukuliwa hatua utawala wa Kizayuni katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. 

Hii ni katika hali ambayo uhusiano kati ya Marekani na Afrika Kusini umedorora sana huku Washington ikiendelea kuufadhili kifedha na kwa silaha utawala haramu wa Israel.

Pandor amekiri kwamba kesi ya mauaji ya kimbari ya Israel imechangia katika kuzorota uhusiano kati ya Pretoria na Washington.