Waasi wa M23 na serikali ya Kinshasa zakubaliana kusitisha mapigano
Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kundi la waasi wa M23 zimetoa taarifa ya pamoja zikieleza kwamba, zimeafikiana kusitisha mapigano mashariki mwa nchi hiyo.
Serikali ya DRC na kundi hilo la waasi zimesema katika taarifa yao hiyo kwamba, kipindi cha usitishwaji wa mapigano kitaendelea wakati huu zikiendelea kuufanyia kazi mchakato wa kuelekea kupatikana kwa mwafaka wa kudumu.
Tangazo hilo linafuatia mazungumzo ya upatanishi yaliyosimamiwa na Qatar ambapo pande zote mbili zilisema "zimekubaliana kufanyia kazi juhudi za kufikia makubaliano" katika mzozo huo ambao umepelekea waasi wa M23 wanaotajwa kuungwa mkono na Rwanda kuteka miji muhimu mashariki mwa nchi hiyo.
Taarifa hiyo imesema pande zote mbili zimethibitisha kujitolea kwao kusitisha mapigano mara moja na kusitishwa uhasama baina yao katika muda wote wa mazungumzo.
Kwa muda mrefu, kundi la M-23 limekuwa likitaka kufanyike mazungumzo ya moja kwa moja na Kinshasa, lakini Rais wa DRC alikataa wito huo, akisema harakati hiyo ni wakala wa Rwanda. Hatimaye, Serikali ya DRC ilikubali kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na kundi hilo nchini Angola mwezi uliopita, lakini M23 ilijiondoa siku moja kabla ya kuanza kwake, kwa sababu eti ya vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya kundi hilo na maafisa wa serikali ya Rwanda.
Tangu Januari mwaka jana, waasi wa M23 wamedhibiti miji ya Goma na Bukavu mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Maelfu ya watu wameuawa na mamia ya maelfu ya wengine wamelazimika kukimbia makazi yao kutokana na mapigano hayo.