Mtaalamu wa sheria Kenya: Uchaguzi wa rais unapaswa kufanyika 2026 na sio 2027 kama ilivyopangwa
-
Willis Otieno
Mtaalamu wa sheria ya uchaguzi wa Kenya amesema kuwa uchaguzi mkuu ujao unapasa kufanyika 2026 na sio 2027.
Katika tafsiri ya kipekee ya Katiba ya Kenya, mtaalamu wa sheria ya uchaguzi, wakili mashuhuri Willis Otieno anasema kwamba, uchaguzi mkuu wa urais ujao unafaa kufanyika Agosti 2026, badala ya 2027 kama inavyopangwa.
Wakili Otieno ameashiria vifungu vya katiba na maamuzi ya awali ya mahakama na kusema, taifa limekuwa likitafsiri vibaya vipindi vya mihula ya rais tangu Katiba ya 2010 ianze kutumika.
“Naleta pendekezo hili nikitambua jukumu la kutetea katiba. Nawaomba Wakenya watekeleze masharti ya katiba kwa uaminifu,” amesema Bw Otieno akizungumza katika kipindi cha Fixing the Nation kwenye runinga ya NTV.
Msingi wa hoja ya wakili Otieno ni kwamba, Katiba ya 2010 iliondoa dhahiri kifungu cha awali kilichotoa muda wa miaka mitano wa muhula wa urais. Badala yake, anasema katiba ya sasa inahitaji uchaguzi kufanyika “katika mwaka wa tano, si baada ya mwaka wa tano” wa muhula wa rais.
Ametoa mfano wa muhula wa kwanza wa Rais wa zamani wa Kenya, Uhuru Kenyatta, ulioendelea kwa miaka minne na miezi mitano badala ya miaka mitano kamili, kama ushahidi kwamba, katiba haijahakikisha muhula wa miaka mitano wa rais.
Tafsiri hii ya katiba huenda ikachochea mjadala mkubwa miongoni mwa wataalamu wa sheria, wachambuzi wa kisiasa na umma kwa ujumla kadiri Kenya inavyokaribia msimu mwingine wa uchaguzi.