Wanachuo wampigisha magoti Trump, awarejeshea viza
Utawala wa Trump umelazimika kuwarejeshea viza maelfu ya wanafunzi wa kigeni wanaosoma nchini Marekani ambao alikuwa amewafutia vibali vya kuishi nchini humo kutokana na kuunga mkono Palestina na kulaani jinai za Israel.
Idara ya mahakama ya Marekani imetangaza kufanyika mabadiliko jumla katika mahakama ya shirikisho baada ya kufanya uchunguzi kuhusu amri kadhaa zilizotolewa na Trump ikiwa ni pamoja na kusimamishwa masomo wanafunzi wa vyuo vikuu na kufutiwa viza zao.
Amri hizo za kusimamishiwa masomo zimezua wasiwasi na hofu kwa maelfu ya wanafunzi ambao walihofia kupoteza haki zao na kufukuzwa haraka nchini Marekani. Wengi walioshtaki kuhusu hatua hizo za Trump wamesema kwamba skuli na vyuo vyao pia vimewazuia kuendelea na masomo au kufanya utafiti huku wengine wakiwa wamebakisha wiki chache tu za kuhitimu masomo.
Mtandao wa Politico wa nchi Marekani umeripoti kuwa, majaji wamechoshwa na hatua hizo za kiholela za Trump na serikali yake hasa kutokana na mawakili wa serikali kutokuwa tayari kusema iwapo wanafunzi hao wanaweza kuendelea na masomo au wanatakiwa kuondoka nchini Marekani mara moja.
Rekodi za wanafunzi zinazojulikana kwa jina la rekodi za SEVIS pia zitarejeshwa kwa wanafunzi waliowasilisha malalamiko yao mahakamani, imesema taarifa hiyo.
Kesi hizo zinaonesha kuwa Idara ya Uhamiaji na Forodha ya Marekani (ICE) ilikuwa ikifuta kumbukumbu za wanafunzi kwa madai kwamba walikuwa na rekodi za uhalifu. Kesi hizo pia zimejumuisha watu ambao walikuwa wamekamatwa na hawakuwahi kushtakiwa au ambao mashtaka yao yametupiliwa mbali.