Wakazi wa Greenland waandamana kupinga vitisho vya Trump
https://parstoday.ir/sw/news/world-i135626-wakazi_wa_greenland_waandamana_kupinga_vitisho_vya_trump
Wakazi wa Greenland walifanya maandamano jana Jumamosi kupinga azma ya Rais wa Marekani Donald Trump ya kutaka kisiwa hicho cha Aktiki kikabidhiwe Washington, wakisisitiza kuwa wakazi wa eneo hilo wanapasa kuachwa waamue mustakabali wa kisiwa hicho.
(last modified 2026-01-18T10:24:38+00:00 )
Jan 18, 2026 10:24 UTC
  • Wakazi wa Greenland waandamana kupinga vitisho vya Trump

Wakazi wa Greenland walifanya maandamano jana Jumamosi kupinga azma ya Rais wa Marekani Donald Trump ya kutaka kisiwa hicho cha Aktiki kikabidhiwe Washington, wakisisitiza kuwa wakazi wa eneo hilo wanapasa kuachwa waamue mustakabali wa kisiwa hicho.

Katika mji mkuu wa Nuuk, mamia ya waandamanaji, wakiongozwa na Waziri Mkuu, Jens-Frederik Nielsen, walibeba bendera na mabango na kukusanyika nje ya ubalozi mdogo wa Marekani.

Waandamanaji hao walielekea katika jengo jipya ambapo Washington inapanga kuhamisha ubalozi wake, ambao kwa sasa na wafanyakazi wanne.

Trump anasema Greenland ni muhimu kwa usalama wa taifa wa Marekani kutokana na kuwepo kwake katika la kistratajia, na hazina kubwa ya madini, na amekuwa akisisitiza mara kwa mara kuwa, ikiazimu, watatumia nguvu kuichukua. 

Hii ni katika hali ambayo, matokeo ya utafiti mpya wa maoni yanaonyesha kuwa ni asilimia 17 tu ya Wamarekani wanaounga mkono juhudi za Trump za kutaka kuiweka Greenland chini ya umiliki wa Marekani. Aidha, idadi kubwa ya wafuasi wa vyama vyote viwili, Democrat na Republican, wanapinga vikali wazo la kutumia nguvu za kijeshi kama njia ya kunyakua kisiwa hicho.

Akthari ya wakazi wa eneo la Greenland wamesema wanahofia kwamba Rais wa Marekani yumkini atatekeleza kivitendo tishio lake la kulitwaa eneo hilo, wakisisitiza kuwa katu hawataki kuwa raia wa Marekani.

Wakazi na viongozi wa eneo hilo wanasisitiza kuwa, kisiwa hicho chenye utajiri wa madini, ambacho kinalinda njia za Aktiki na Bahari ya Atlantiki Kaskazini kuelekea Amerika Kaskazini, "ni milki ya watu wake."