Kukiri kufeli operesheni ya kijeshi ya Marekani nchini Yemen
Wiki kadhaa zimepita tangu Marekani ilipoanzisha operesheni kubwa na tata za kijeshi dhidi ya Yemen, huku kukiwa na mashambulizi ya mara kwa mara na mengi ya anga katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo, lakini hivi sasa vyombo vya habari vya Marekani vimekiri kushindwa utawala wa Trump katika operesheni zake za kujeshi huko Yemen.
Gazeti la Foreign Policy la Marekani liliandika tarehe 22 Aprili katika makala yenye kichwa cha habari "Vita vya Trump dhidi ya Wahouthi Havifiki Popote," ikiashiria mashambulizi yasiyo na matunda ya Jeshi la Wanamaji la Marekani dhidi ya vikosi vya Ansarullah vya Yemen kwamba: Wiki tano baada ya utawala wa Trump kuzidisha mashambulizi yake dhidi ya Wahouthi, matatizo kadhaa makubwa yamejitokeza, jambo linaloashiria kuwa itamuwia vigumu sana Trump kuyafanya majigambo yake kuhusu Yemen yazae matunda.
Kwa mujibu wa chapisho hilo, hadi hivi sasa mashambuklizi ya Marekani nchini Yemen yameshindwa kufanikisha angalau moja ya malengo yake mawili yaliyotangawa na Trump ambayo ni: Kufungua njia za Bahari Nyekundu kwa ajili ya meli za Marekani na zinazoelekea Israel na pili kuzuia Yemen isishambulie maeneo ya utawala wa Kizayuni. Usafirishaji wa vyombo vya baharini kupitia Bahari Nyekundu na Mfereji wa Suez bado uko chini licha ya mashambulizi ambayo kuitia hasara Marekani ya zaidi ya dola bilioni moja hadi hivi sasa. Wanamapambano wa Yemen pia wamezidisha mashambulizi yao dhidi ya Israel na meli za kivita za Marekani na kumuonya Trump kwamba amejiingiza kwenye kinamasi cha matope ya Yemen.

Mahdi Al-Mashat, Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Kisiasa na Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Ulinzi la Yemen alisema tarehe 20 Aprili kwamba: "Mashambulio ya Marekani dhidi ya Yemen yalishindwa tangu siku ya kwanza. Marekani itaadhibiwa kwa vitendo vinavyokiuka mikataba ya kimataifa. Trump anataka kutuzamisha kwenye kinamasi, lakini tunapaswa kumwacha abaki humo yeye mwenyewe. Wananchi wa Marekani wanapaswa kujua kwamba Trump amewaletea aibu na kwamba Marekani imeshindwa huko Yemen tangu siku ya kwanza."
Jarida la Foreign Policy limeongeza kuwa, kuna ukosefu wa uwazi kuhusu operesheni za Marekani nchini Yemen licha ya kwamba hayo ni mashambulizi makubwa zaidi ya kijeshi ya Marekani katika muhula wa pili wa Trump. Wizara ya Ulinzi ya Marekani haijatoa maelezo yoyote kuhusu vita vinavyoendelea, na Komandi Kuu ya Marekani (CENTCOM) huchapisha tu video za kuchochea hisia za watu ambazo zinaonesha ndege za kivita zikipaa kutoka kwenye manuwari za Marekani.

Jarida hilo la Marekani limesisitiza kwa kuandika: "Jambo linalotia wasiwasi zaidi kuliko masuala yaliyotajwa hapo juu ni matumizi makubwa ya silaha za kisasa zinazoongozwa kwa usahihi kabisa katika mashambulizi ya usiku na mchana ya manuwari mbili za kubeba silaha za Marekani yaani Harry Truman na Carl Vinson. Wachambuzi wa masuala ya kijeshi wanasema kuwa, kama hali ni hiyo huko Yemen, je hali itakuwaje iwapo Marekani itaingia vitani na nchi kama China? Suala hili ni muhimu hasa kutokana na kwamba Marekani imeipa Taiwan idadi ndogo tu ya makombora licha ya kwamba nchi hiyo itayahitajia sana makombora ya kurushwa hewani kama kutazuka vita kati yake na China.
Kwa upande mwingine, suala la kufunguliwa njia za Bahari Nyekundu ni muhimu mno hivi sasa na udharura wake ni wa haraka zaidi kuliko wakati mwingine wowote. Bahari Nyekundu na Mfereji wa Suez ni maeneo muhimu mno kwa safari za kibiashara hasa kwa kuzingatia kuwa vita vya biashara vilivyoanzishwa na Trump vimelitia kwenye giza suala zima la usafirishaji wa meli ulimwenguni. Mashirika ya usafirishaji bidhaa kwa njia ya bahari hayataki kula hasara ya kwenda safari ndefu ya kuzunguka bara la Afrika wakati njia ya mkato sana ipo nayo ni ya Bahari Nyekundu na Mfereji wa Suez hususan wakati huu ambapo Trump ameanzisha vita vya ushuru kwa bidhaa za mataifa mbalimbali duniani.

Kukiri jarida maarufu la Foreigh Policy la Marekani, ambalo linaakisi mitazamo ya wasomi wa kisiasa wa nchi hiyo, kwamba Trump ameshindwa kwenye mashambulizi yake huko Yemen, kunaonyesha kwamba, licha ya Trump kujifanya hajali na pamoja na kwamba anatoa majigambo ya kila namna, lakini mshindi ni taifa la Yemen ambalo lina uzoefu wa vita vya miaka minane vya pande zote vilivyoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya taifa hilo la Kiislamu, lakini lilisimama imara. Hivi sasa pia taifa la Yemen halitetereki katika msimamo wake wa kuwaunga mkono Wapalestina na madhali mashambulizi ya Israel hayajakomeshwa huko Ghaza, hakuna kitu ambacho kitawakinaisha Wayemen wakubali kufungua njia za Bahari Nyekundu.