Hatua mpya katika kuzidisha kiwango cha ushirikiano kati ya Iran na Russia
(last modified Sat, 26 Apr 2025 10:50:15 GMT )
Apr 26, 2025 10:50 UTC
  • Hatua mpya katika kuzidisha kiwango cha ushirikiano kati ya Iran na Russia

Miamala ya kibiashara kati ya Iran na Russia inazidi kuongezeka katika nyanja mbalimbali za kiuchumi hususan katika sekta ya nishati na usafirishaji.

Mohsen Paknejad, Waziri wa Mafuta wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeleza matarajio yake kwamba,  kupitia ushirikiano wa Iran na Russia na kuondolewa vikwazo na changamoto zilizopo za kimifumo; uhusiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili utaongezeka na kufikia kiwango kinachostahiki kwa nchi mbili. Waziri wa Mafuta wa Iran ameeleza haya katika mkutano wa 18 wa Kamisheni ya Pamoja ya Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Iran na Russia mjini Moscow, Russia. 

Mohsen Paknejad pia ameashiria Mkataba Ushirikiano Kamili wa Kistratejia uliotiwa saini na viongozi wa Iran na Russia miezi kadhaa iliyopita na kupasishwa kwake na kusema, hiyo ni hatua muhimu katika kuimarisha  uhusiano wa pande mbili katika kiwango kipya cha uhusiano wa muda mrefu na wa kimkakati. 

Iran na Russia zinafanya juhudi kuimarisha uhusiano wa kibiashara na kuzidisha kiwango cha sasa kutoka thamani ya dola bilioni 5 na kufika zaidi ya dola bilioni 10 kwa mwaka. Rasilimali nyingi za nchi hizo mbili hususan katika uga wa nishati, na ukaribu wa kijiografia kwa upande mmoja, na mashinikizo ya nchi za Magharibi na vikwazo vya kiuchumi na kisiasa vya nchi hizo dhidi ya Iran na Russia kwa upande mwingine, vimekuwa sababu ya nchi mbili kujikita zaidi katika kuzidisha ushirikiano wao wa kiuchumi. 

Kuhusiana na suala hili, jumbe za kiuchumi za Iran na Russia, siku kadhaa zilizopita, zilikuwa na kikao cha pamoja cha kiuchumi huko Russia ili kuchunguza namna ya kushirikiana hasa katika nyanja mbalimbali za nishati, masuala ya fedha na benki, kilimo na kusaini mapatano mapya katika uwanja huo.

Waziri wa Mafuta wa Iran amesema: Mapatano yaliyofikiwa yameainisiha fremu ya ushirikiano wa muda mrefu kati ya nchi mbli, na Wizara ya Mafuta ya Iran itafuatilia kwa jadi utekelezaji wa mapatano hayo. 

Sekta ya nishati ni moja ya maneo yenye umuhimu mkubwa kwa ajili ya kuimarisha ushirikiano kati ya Iran na Russia. Nchi mbili hizi ambazo ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa mafuta na gesi duniani na zimewekewa vikwazo, zinajaribu kupanga ajenda yao ya kazi ndani ya fremu ya ushirikiano wa kikanda na kufikia mapatano ya kubadilishana teknolojia ya kisasa, uwekezaji wa pamoja katika nyanja za mafuta na gesi za Iran na kushirikiana katika miradi mbalimbali ya kuuza nje nishati.  

Kampuni ya nishati ya Russia ya Gazprom

Mbali na sekta ya nishati, Iran na Moscow zinaweza kushirikiana katika pande kadhaa katika nyanja za usafirishaji, mradi wa ushoroba wa Kaskazini- Kusini unaounganisha Iran na Russia na kuendelea hadi Ulaya na India. Wakati huo huo kuimarishwa miundombinu ya reli, barabara na bandari nchini Iran kwa uwekezaji wa Russia ni hatua muhimu kuelekea kkwenye utekelezaji wa mradi huu wa kimkakati.

Suala jingine linalofuatiliwa na nchi mbili ni kuhusu kutumiwa sarafu za kitaifa za nchi hizo katika malipo, au kwa maneno mengine, kuweka kando matumizi ya sarafu ya dola ya Marekani katika miamala ya kibiashara kati ya nchi mbili. Jambo hili, ambalo linatajwa kuwa hatua kubwa ya kukabiliana na vikwazo vya kifedha vya Marekani na washirika wake, litazamiwa kupewa kipaumbele maalumu katika ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tehran na Moscow.

Kwa upande wa kisiasa pia Iran na Russia zinasisitiza kuwa zinapinga mfumo wa kambi moja wa Magharibi. Hii ni katika hali ambayo, Iran imekuwa mwanachama katika Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai na katika kundi la BRICS kwa uungaji mkono wa kisiasa wa Russia. Wakati huo huo kuwa pamoja nchi mbili katika aghalabu ya masuala ya kikanda na kimataifa kunaashiria azma thabiti ya Tehran na Moscow ya kuwa na nafasi kuu katika kuasisi mfumo mpya wa dunia. 

Nchi za BRICS 

Katika mazingira haya ya sasa inaonekana kuwa, kama miradi iliyoainishwa itatekelezwa ipasavyo, basi uhusiano kati ya Iran na Russia unaweza kuingia katika hatua ya "ushirikiano endelevu."

Kwa ujumla, matokeo ya kikao cha 18 cha Kamisheni ya Pamoja yanadhihirisha wazi kwamba ushirikiano kati ya Iran na Russia uko katika muktadha wa ukuaji na mwingiliano, na mustakbali unaonekana kuwa mzuri kwa ushirikiano na usimamizi makini wa nchi hizo mbili, japokuwa mafanikio haya pia yatakabiliwa na changamoto.