UN yatahadharisha kuhusu hali mbaya za wakimbizi wa Kongo wanaoingia Burundi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i125646-un_yatahadharisha_kuhusu_hali_mbaya_za_wakimbizi_wa_kongo_wanaoingia_burundi
Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limesema kuongezeka idadi ya wakimbizi wanaokimbia mzozo mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwenda Burundi kunaweka "shinikizo kubwa kwa mashirika ya misaada yanayojitahidi kukabiliana na mzozo unaozidi kuwa mbaya huku kukiwa na uhaba wa rasilimali."
(last modified 2025-04-26T03:04:31+00:00 )
Apr 26, 2025 03:04 UTC
  • UN yatahadharisha kuhusu hali mbaya za wakimbizi wa Kongo wanaoingia Burundi

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limesema kuongezeka idadi ya wakimbizi wanaokimbia mzozo mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwenda Burundi kunaweka "shinikizo kubwa kwa mashirika ya misaada yanayojitahidi kukabiliana na mzozo unaozidi kuwa mbaya huku kukiwa na uhaba wa rasilimali."

Shirika hilo limeongeza katika taarifa yake iliyotolewa jana Ijumaa kuwa zaidi ya watu 71,000 wamevuka mpaka na kuingia Burundi tangu mwanzoni mwa mwaka huu, wakikimbia ghasia zinazoendelea mashariki mwa Kongo.

UNHCR imeongeza kuwa zaidi ya wakimbizi 12,000 wamehamishiwa kwenye eneo la Musini, huku wengine wakiishi na jamii zinazowapokea katika maeneo ya mpakani.

UNHCR imesema eneo la Musini, karibu na mpaka wa nchi hizo mbili, limejaa watu na lina takriban watu 16,000 licha ya kuwa limetayarishwa kuhifadhi watu 3,000 pekee.

Mkurugenzi wa Dharura wa UNHCR ameeleza kuwa mgogoro wa binadamu katika mpaka wa Burundi na Kongo DR hauishii kwenye uhaba wa chakula, kwani maji ya mvua yamefurika mahema ya dharura yaliyowekwa katika ardhi ya uwanda wa kilimo, na hivyo kuzidisha hatari ya kusambaa magonjwa. 

Tangu Januari mwaka jana, eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limekumbwa na mapigano makali kati ya waasi wa M23 na vikosi vya serikali, na hadi sasa maelfu ya watu wameuawa na makumi ya maelfu wengine wamelazimika kuyahama makazi yao.